Na mwandishi wetu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro ameutaka uongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) kuendeleza programu muhimu za mchezo huo ikiwemo kung’amua vipaji kutoka shuleni.
Dk Ndumbaro pia amewataka viongozi hao kusimamia vizuri maandalizi ya timu ya taifa ili iweze kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Waziri huyo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam leo Alhamisi alipofanya kikao na uongozi wa Chaneta katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo pia alisisitiza kutoendekeza migogoro bali kuwa na umoja na mshikamano kwa maslahi ya mchezo wa netiboli.
“Viongozi mliopo kwa maslahi ya mchezo wa netiboli Tanzania, si vyema mkaendekeza migogoro katika chama, bali mnapaswa kuendeleza programu muhimu zilizopo, ikiwemo kung’amua vipaji kutoka mashuleni hususani katika mashindano ya shule za msingi na sekondari,” alisema Dk Ndumbaro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chaneta, Dk Devotha Marwa ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na serikali pamoja na kuendelea kukiongoza chama kwa weledi zaidi.
“Nashukuru kwanza kwa Waziri kukutana na uongozi wa Chaneta, namuahidi nitatekeleza maagizo yote na kukiongoza chama kwa weledi.”
