Na mwandishi maalum
Watanzania wana mengi ya kujifunza kutoka kwa rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi ‘Mzee Rukhsa’, moja kati ya hayo ni utamaduni wa kufanya mazoezi.
Kwa mara ya kwanza nilibaini kuwa Mzee Rukhsa ni mtu wa mazoezi miaka ya 2000 mwanzoni, siku niliyofika kwa mara ya kwanza nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam majira ya asubuhi.
Siku hiyo kulikuwa na tukio la uzinduzi wa mashindano ya soka ya Mufindi, tukio ambalo lilifanyika asubuhi nyumbani kwake, tukiwa hapo na wenzangu tuliambiwa tusubiri kidogo mzee alikuwa kwenye mazoezi.
Baadhi yetu walishangaa kusikia hivyo kutokana na umri wake kwa imani kwamba tungemkuta akiwa amejipumzisha au amelala na si kufanya mazoezi.
Baada ya kama nusu saa hivi Mzee Rukhsa aliwasili na ratiba fupi ya tukio lile ikaendelea kama kawaida ikihusisha waandaaji, waandishi wa habari na watu wengine wachache.
Ukiachana na tukio hilo, Mzee Rukhsa ambaye amefariki dunia Februari 29, 2024, suala la mazoezi lilikuwa wazi kwa kila Mtanzania aliyefuatilia matukio mbalimbali yaliyomhusisha.
Leo hii kiongozi huyu amefariki akiwa na miaka 98 lakini wengi wetu tumemshuhudia akiwa na miaka 80 na hata 90 akifanya mambo ambayo wapo baadhi ya vijana wa miaka 20, 30, 40 na hata watu wazima wa miaka 50 hawawezi kufanya.
Moja ya jambo hilo ni kutembea umbali mrefu, tumemshuhudia Mzee Rukhsa akishiriki matembezi mbalimbali ya hisani ya kuanzia kilometa moja, mbili wakati mwingine hadi tano na kumudu kutembea bila kuonesha uchovu wa aina yoyote.
Uzee wake wakati wote haukuwa tatizo, alitembea bila wasiwasi na kumaliza mwendo, lakini leo nina hakika kuna vijana wengi tu wa umri nilioutaja hapo juu ambao ukimwambia atembee kilometa mbili au tatu mtagombana, ni ama hawezi au hayuko tayari.
Katika hili hatuna sababu ya kukumbashana kauli za mara kwa mara za madaktari kututaka tuwe na utamaduni wa kufanya mazoezi yakiwamo yale ya kutembea badala yake Mzee Rukhsa anatosha kabisa kuwa somo katika hili.
Huenda kutokana na mazoezi ndio maana amekuwa mwenye nguvu na imara wakati wote licha ya umri wake kuwa mkubwa na hakuonesha dalili zozote za uchovu kama ambavyo ingekuwa kwa mzee wa umri wake.
Na hapa pia tunaweza kukumbushana tukio la kuvamiwa na mtu jukwaani kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee na kupigwa, Mzee Rukhsa katika tukio hili japo lilikuwa baya na lililofedhehesha wengi lakini alituonesha jinsi alivyokuwa ‘fiti’.
Hakuweweseka kama ambavyo ingetarajiwa kwa mzee wa umri wake, badala yake alijaribu kujihami na hata baada ya maofisa usalama kuingilia kati Mzee Rukhsa alikuwa wa kwanza kutumia kipaza sauti kuwatoa watu hofu aliposema, “Babu yenu nipo salama, msihofu.”
Tatizo pekee ambalo wengi wetu tulilishuhudia kwa Mzee Rukhsa ni kusahau, hili alilisema wakati wa mazishi ya Rais John Magufuli mwaka 2021, lakini ukiacha tatizo hilo bado kwa muonekano alionekana kuwa imara na mwenye afya njema licha ya kuwa na umri kuwa mkubwa.
Kwa hiyo ni kweli kwamba tuna mengi ya kujifunza kwa Mzee Rukhsa, mojawapo ni hili la mazeoezi, madaktari wanatuhimiza kila mara kufanya mazoezi, Mzee Rukhsa ametupa faida yake, anabaki na ataendelea kuwa mfano bora wa umuhimu wa mazoezi kwa afya zetu.
Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.