Doha, Qatar
Manahodha wawili, Lionel Messi wa Argentina mwenye miaka 35 na Luka Modric wa Croatia mwenye miaka 37, leo watapambana katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia huku wakifahamu kwamba uwezekano wa kushiriki fainali zijazo ni mdogo au haupo.
Katika fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026, Messi atakuwa na miaka 39 na Modric miaka 41, kimsingi kwa wachezaji hao mechi ya leo ina maana kubwa katika kuhakikisha wanaziaga vyema timu zao za Taifa wakiwa mashujaa kwani itakuwa mechi ya mwisho ya fainali za Kombe la Dunia kwa yeyote ambaye timu yake itatolewa.
Hadi sasa Messi na Modric ambao wote wana tuzo (Ballon d’Or) kwenye makabati yao japo Messi ana tuzo nyingi (saba) kumzidi Modric, wameshaonyesha dhamira yao ya kuhakikisha wanaweka historia kwa namna ambavyo wamezisaidia timu zao hadi kufikia nusu fainali hii leo.
Mechi ya leo ndiyo iliyobeba jibu la nani kati ya Messi na Modric ambaye Jumapili atakuwa uwanjani na timu yake ya taifa akicheza mechi ya fainali dhidi ya Ufaransa au Morocco?
Mchango wa wachezaji hao wawili kwa timu zao kwenye fainali za Kombe la Dunia si kitu kigeni, mwaka 2014, mchango mkubwa wa Messi uliifikisha Argentina katika fainali nchini Brazil kabla ya kupoteza mechi mbele ya Ujeumani kwa bao 1-0 na mwaka 2018 Modric naye alifanya hivyo hivyo nchini Urusi, Croatia ililala mbele ya Ufaransa kwa mabao 4-2.

Kwa hiyo Messi na Modric leo wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kulikosa Kombe la Dunia, Messi atakumbuka ya 2014 na Modric atakumbuka mambo ya 2018, wote wakiwa wamefanya kazi kubwa kwa timu zao kwenye fainali za 2022 hadi leo wanakutana hatua ya nusu fainali.
Hadi kufuzu hatua ya nusu fainali, Argentina iliitoa Uholanzi kwa penalti wakati Croatia nayo iliitoa Brazil pia kwa penalti, Messi alipiga penalti ya kwanza ya Argentina wakati Modric alipiga ya tatu, wote walifunga penalti zao.
Mechi ya leo kwa Messi itakuwa inamkumbusha bao lake la kwanza na timu ya Taifa ya Argentina, bao ambalo alilifunga katika mechi ya kirafiki dhidi ya Croatia Machi 2006 wakati kwa Modric mechi hiyo inamkumbusha siku alipoichezea kwa mara ya kwanza timu ya Taifa ya Croatia ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Nje ya takwimu hizo, mashabiki wa Argentina na Croatia nao hawako nyuma, wanaendelea kuongeza hamasa ya mechi ya leo kwa namna ambavyo wamekuwa na mabango na jezi zenye majina ya Messi na Modric.
