Na mwandishi wetu
Mchezaji mpya wa Yanga Princess, Kaida Wilson raia wa Marekani amesema ana furaha kujiunga na timu hiyo akiahidi kufanya vizuri kuisaidia kufikisha malengo yake.
Mchezaji huyo, 17, alisema yupo Yanga kucheza kwa msimu mmoja hadi mwakani ataondoka kurudi Marekani kwa ajili ya kuendelea na masomo.
“Nina furaha kuwa hapa na naamini nitapata wakati mzuri wa kuisaidia timu pale nitakapopata nafasi, mimi ninacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na niko hapa kupambana. Kidogo napata changamoto ya jua kali lakini taratibu naanza kuzoea ili kwenda sawa na wenzangu,”alisema.
Mratibu wa timu hiyo, Kibwana Matokeo aliyemuunganisha kiungo huyo na Yanga, alisema baba mzazi wa mtoto huyo alivutiwa na Yanga na ndipo akatamani mtoto wake aje kuitumikia Yanga Princess.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kulingana na usajili wa wachezaji waliofanya msimu huu, anaamini timu hiyo itarudi katika ushindani kwenye Ligi Kuu ya Wanawake na kufanya vizuri ikiwezekana kutwaa ubingwa.
