London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amewakingia kifua wachezaji wake waliojiweka kando na timu zao za taifa akidai kuwa klabu yao ina uhusiano mzuri na timu hizo licha ya uamuzi wa wachezaji hao.
Katika mechi za hivi karibuni za timu za taifa wachezaji 228 kutoka timu 20 za Ligi Kuu England waliitwa kwenye timu zao za taifa kwa mechi za kirafiki, kati yao 23 walijitoa katika mechi hizo wengi wao wakiwa wa Arsenal.
Kitendo cha wachezaji wa Arsenal kutoungana na wenzao kwenye timu za taifa kimeibua uvumi kwamba uamuzi huo huenda unatokana na janga la wachezaji majeruhi katika timu hiyo au hofu ya wachezaji wengine kupata majeraha.
Arteta hata hivyo alipingana na mtazamo huo na kubainisha kuwa hali ya kiafya na uwapo wa wachezaji majeruhi vyote viliwekwa wazi kwa viongozi wa timu zao za taifa.
“Tuna uhusiano mzuri na tunawasiliana na timu karibu zote za taifa hasa kocha wa England, Thomas (Tuchel), tumekuwa tukiwapa ushirikiano wakati wote, tunapowasilisha taarifa kuhusu hali ya kila mchezaji tunakuwa wakweli na uamuzi unafikiwa kwa kuzingatia ripoti ya madaktari na baada ya hapo ndipo tunapofikia uamuzi wa mwisho,” alisema Arteta.
Baada ya Arsenal kushindwa kutamba mbele ya Man City kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Carabao, beki William Saliba aliweka wazi kuwa hatoungana na wenzake kwenye timu ya taifa ya Ufaransa kwa sababu ya majeraha ya enka.
Wachezaji wengine waliochukua uamuzi kama wa Saliba ni beki mwenzake Gabriel aliyejitoa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kwa tatizo la goti pamoja na Bukayo Saka, Declan Rice na Noni Madueke waliojitoa kwenye timu ya England, Martin Zubimendi (Hispania) na Piero Hincapie (Ecuador).
Wengine waliotosa sababu za kuwa majeruhi na timu zao za taifa kwenye mabano ni Eberechi Eze (England), Martin Odegaard (Norway), Jurrien Timber (Uholanzi), Leandro Trossard (Ubelgiji).
