London, England
Wakati Ligi Kuu NBC ikijivunia uwapo wa mwamuzi mwanamke, Jonesia Rukyaa, Ligi Kuu England (EPL) inatarajia kuweka rekodi hiyo, Desemba 23 wakati Rebecca Welch (pichani) atakapokuwa mwamuzi wa kwanza mwanamke kuchezesha mechi ya EPL kati ya Fulham na Burnley.
Rebecca, 40, ambaye Januari mwaka huu alijiwekea rekodi ya kuwa mwamuzi wa kwanza mwanamke kuchezesha mechi za ligi ya Championship, alianza kazi ya uamuzi mwaka 2010.
Rekodi nyingine ya waamuzi wa EPL inatarajia kuwekwa na Sam Allison katika kipindi hiki hiki cha Desemba ambaye atakuwa mwamuzi wa kwanza mweusi mwenye asili ya Afrika kuchezesha mechi ya EPL katika kipindi cha miaka 15 atakapochezesha mechi kati ya Luton na Sheffield United ambayo itapigwa Desemba 26.
Kiongozi mkuu wa waamuzi wa EPL, Howard Webb ambaye ni mwamuzi wa zamani wa kimataifa alisema kwamba Rebecca na Sam ni waamuzi wa hadhi ya uhakika.
“Hii ni hatua muhimu kwa Rebbeca na Sam ambao ni waamuzi wawili wa hadhi ya uhakika, wana haki ya kupewa fursa hiyo,” alisema Webb.