Na mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Kampuni ya PAF Promotion Entertainment, Godson Karigo amesema yupo kwenye hatua za mwisho kuhakikisha anampeleka mahakamani bondia Hassan Mwakinyo kwa madai ya kukiuka mkataba baina yao.
Akizungumza leo Alhamisi na GreenSports, Karigo alisema mbali na mkataba unaolenga fidia ya hasara waliyoipata baada ya bondia huyo kugoma kupanda ulingoni Septemba 29, mwaka huu, pia maneno ya kashfa anayodai kutolewa na bondia huyo dhidi yake.
“Tunafanya taratibu za kulifikisha hili suala mahakamani, tunataka fidia ya kilichopotea na matusi tuliyotukanwa kurugenzi na kampuni nzima kuchafuliwa, maana ametuita sisi wababaishaji, tunadhulumu mabondia na mengi kama hayo,” alisema Karigo.
Na ingawa Karigo hakuwa tayari kuweka wazi alipoulizwa kuhusiana na gharama ya fidia wanayokwenda kudai lakini GreenSports inafahamu ni kiasi cha fedha zaidi ya Shilingi milioni 500 kama ilivyoelezwa na chanzo kutoka ndani ya PAF.
“Bado tunafanya hesabu kuhusu hiyo fidia, tutaeleza hesabu kamili ni ipi lakini kwa sasa bado tunaendelea na mchanganuo kisha tutaweka wazi baada ya kumaliza mchakato wa kesi ndani ya siku mbili tatu hizi,” alisema Karigo.
Karigo ameamua kufanya hivyo ikiwa ni siku tatu zimepita tangu Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kumfungia Mwakinyo kwa mwaka mmoja na kumtoza faini ya Shilingi milioni moja kwa kosa la kutopanda ulingoni siku hiyo na kukiuka mkataba wake huo.