London, England
Kocha wa Tottenham Hotspur, Antonio Conte jana Alhamisi alirudi kazini na kuendelea na majukumu yake baada ya kufanyiwa upasuaji wa kibofu.
Conte alifanyiwa upasuaji huo nyumbani kwao Iralia wiki iliyopita baada ya kuwa na maumivu kwenye tumbo na hivyo kuikosa mechi ya Jumapili iliyopita ambayo timu yake iliichapa Man City bao 1-0.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53, alirejea jijini London juzi Jumatano lakini hadi sasa haijaweza kufahamika mara moja kama atakuwa kwenye benchi kesho Jumamosi wakati Spurs itakapokuwa ugenini dhidi ya Leicester.
“Ni lazima ajitulize kwa muda, asijichoshe lakini tuna furaha kukutana naye kwa mara nyingine kwenye uwanja wa mazoezi, leo (jana) asubuhi alikuwa uwanjani pamoja nasi,” alisema kocha msaidizi, Cristian Stellini akimzungumzia Conte aliyetua Spurs mwaka 2021 akitokea Inter Milan.
“Alitumia muda mwingi akisalimiana kwa kukumbatiana na kila mtu, hakuzungumza chochote kuhusu atafanya nini baada ya hapo lakini kimsingi amerudi na tuna furaha,” aliongeza Stellini.
Stellini ambaye ndiye aliyeiongoza timu hiyo katika mechi dhidi ya City pia alimzungumzia kipa wao majeruhi aliyeumia goti, Hugo Lloris akisema kwamba atakosekana uwanjani kwa wiki tano hadi sasa.
Kocha huyo msaidizi pia alikataa kuzungumza chochote kuhusu mambo ya baadaye ya Conte katika klabu hiyo. Mkataba wa Conte unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu ingawa ana nafasi ya kuongeza miezi mingine 12.
“Hatukuwahi kuzungumzia hilo la mkataba, katika soka huwezi kutulia kwa sababu tu una mkataba au hauna, ni lazima ufanye kazi kwa bidii, huwezi kubweteka, unaishi ukiwa na nguvu kwa kuwa unataka kushinda, kwa hiyo huna muda wa kuzungumzia mambo yako yajayo,” alisema.
“Haya ndiyo maisha yetu, hii ni soka, ni mchezo, unafikiria lengo lijalo unalotaka kulifanikisha, unachotaka kufanikisha ni hilo kwa hiyo hubweteki, uwe na mkataba au usiwe nao,” alifafanua.