Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Felix Minziro amesema bado hafahamu hatma yake ya kuendelea kuinoa timu hiyo kutokana na kufika ukingoni kwa mkataba wake.
Kocha huyo ameiambia GreenSports leo Ijumaa kuwa mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, ingawa amepata ofa za timu nyingine tayari lakini anasikiliza kwanza mazungumzo ya mabosi wake hao wa sasa.
Amesema ingawa anatarajia kukutana na uongozi wa timu hiyo hivi karibuni kufahamu kama anaendelea au la lakini kutokuwa na uhakika kwa sasa kunamkwamisha kuanza harakati za mapema za kufanya usajili wa wachezaji wa msimu ujao.
“Ni kweli namaliza mkataba mwisho wa msimu huu, zimesalia siku chache mno lakini bado hakuna mazungumzo na uongozi kuhusiana na hilo japokuwa natarajia kukutana nao kabla ya kucheza mechi mbili zilizosalia za ligi.
“Kama inavyoonekana kweli tunaelekea kipindi cha usajili, kuisuka vizuri zaidi timu kwa ajili ya msimu ujao lakini huwezi kufanya hivyo kwa sasa sababu bado haijafahamika itakuwaje siku za usoni kuhusu kuendelea kubaki Geita,” alisema Minziro.
Minziro beki wa zamani wa Yanga, amekuwa na Geita tangu alipoipandisha timu hiyo daraja kucheza ligi kuu msimu wa 2021-22 na kisha kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hiyo ni baada ya kumaliza kwenye nne bora ya msimamo wa ligi kuu katika msimu wao wa kwanza. Msimu huu Geita ipo nafasi ya sita ikipambana kumaliza kwenye tano bora.