Na mwandishi wetu
Simba imefuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la FA (Azam Sports Federation) kwa kishindo ikiitandika TRA Kilimanjaro mabao 6-0 katika mechi iliyopigwa Jumatano hii usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba katika mchezo huo alikuwa ni Sadio Kanoute ambaye aliifungia timu hiyo mabao matatu peke yake au hat trick katika dakika za 39, 54 na 55.
Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Ladack Chasambi aliyefungua karamu ya mabao hayo katika dakika ya 13 na mengine mawili yalifungwa na Freddy Kouablan dakika ya 51 na Pa Omar Jobe katika dakika ya 71.
TRA ilifikia hatua ya kucheza na Simba baada ya kuitoa Tanzania Prisons ya Mbeya inayoshiriki Ligi Kuu NBC kwa mikwaju ya penalti 6-5, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Kwa upande wa Simba wao waliibuka na ushindi mwingine mnono wa mabao 4-0 katika mechi yake na Tembo FC, mechi ambayo pia ilichezwa Azam Complex.