Na mwandishi wetu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro ameipongeza timu ya Taifa ya mchezo wa gofu ya wanawake kwa kutetea ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano iliyofanyika Kigali, Rwanda kuanzia Novemba Mosi hadi 3, mwaka huu.
Dk Ndumbaro alitoa pongezi hizo katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam baada ya timu hiyo kupeleka makombe hayo ofisini kwake leo Jumatano.
“Hakika nimejionea mambo makubwa na yenye kuvutia zaidi kwa wachezaji wetu wa mchezo wa gofu kwa wanawake nchini, wametuheshimisha kwa kuonesha mchezo mzuri na kuliheshimisha taifa letu.
“Rekodi yetu ni mara ya nne kwa timu ya mchezo wa gofu kwa kutuletea heshima hapa nchini na wizara tunawahakikishia kwamba tutaendelea kuwa nanyi kwa kila kitu, kwa hii heshima kwetu kama Watanzania,” alisema Dk Ndumbaro.
Naye nahodha wa timu hiyo, Hawa Wanyeche aliishukuru serikali kwa kuonesha umoja na timu yao kuwa katika hali nzuri kitu ambacho kiliwapa hamasa kubwa na kucheza kwa wakiwa na ari.
“Hakika upinzani ulikuwa mkali lakini sisi tulihakikisha kuwa tunajitoa kwa moyo ili sisi wawakilishi pekee kutoka hapa Tanzania kuhakikisha tunaiwakilisha nchi na hakika Mungu ametutangulia na kuibuka mabingwa kati ya nchi saba,”
“Kiujumla mchezo ulikuwa mzuri na wa kipekee na tumeweza kuiwakilisha nchi na kurudi na kombe,” alisema Hawa akiwawakilisha wachezaji wengine wa timu hiyo; Neema Olomi, Vicky Elias na Madina Iddi.