London, England
Man City imebeba taji la Ligi Kuu England kwa kishindo baada ya kuilaza Aston Villa mabao 3-2 na kuitibulia Liverpool malengo yake ya kuweka rekodi ya kubeba mataji manne kwa msimu mmoja.
Liverpool ingefanikiwa kulibeba taji hilo leo, lingekuwa taji lao la tatu msimu huu, tayari wana taji la FA, la Ligi huku wakisubiri Jumamosi ijayo kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya watakapoumana na Real Madrid katika mechi ya fainali.
Haikuwa rahisi kwa City kulibeba taji hilo hasa baada ya kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Aston Villa inayonolewa na kiungo na nahodha wa zamani wa Liverpool, Steven Gerarrd ambaye iliaminika angeiandaa timu yake kuidhibiti City ili kuirahisishia Liverpool kazi ya kulibeba taji hilo.
Villa ndio waliokuwa wakiongoza mechi hiyo na ilihitajika ubabe wa City kupindua matokeo baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 na hivyo ikawalazimu City kusawazisha na kuongeza bao moja.
Kabla ya mechi hiyo City walikuwa wameizidi Liverpool kwa tofauti ya pointi moja, City walikuwa na pointi 90 wakati Liverpool walikuwa na pointi 89 lakini ushindi wa mechi zao za mwisho umeifanya City ifikishe pointi 93 dhidi ya 92 za Liverpool ambayo iliilaza Wolves mabao 3-1.
Villa ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 37 lililofungwa na Cash na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Villa wakiwa mbele kwa bao hilo kabla ya kuongeza la pili dakika 25 baada ya mapumziko kwa bao lililofungwa na Coutinho.
City walipambana na kupata bao la kwanza dakika ya 76 lililofungwa na Gundogan kabla ya kusawazisha dakika mbili baadaye kwa bao lililofungwa na Rodri na hivyo kuzifanya timu hizo ziwe sare hali iliyoanza kuibua matumaini ya City kupoteza taji huku Liverpool iliyokuwa ikiumana na Wolves ikianza kujipa matumaini kwani hadi wakati huo timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1 huku Liverpool ikionyesha kila dalili za kutoka uwanjani na ushindi.
Bao la Liverpool lilifungwa na Mane dakika ya 24 baada ya Wolves kutangulia kupata bao dakika ya nne lililofungwa na Neto lakini matumaini yao yalizimika baada ya Gundogan kuipatia City bao la tatu katika dakika ya 81 na hivyo City kumaliza mechi yao na Villa wakiwa washindi kwa mabao 3-2. Ushindi mgumu lakini ulitosha kuwapa taji.
Kwa upande mwingine Liverpool nao waliongeza mabao mawili katika dakika za 84 na 89 wafungaji wakiwa ni Mohamed Salah na Robertson, mabao ambayo hayakuwasaidia kutwaa taji la Ligi Kuu England ingawa kwa Salah bao lake lilikuwa na maana kubwa kwani lilimuwezesha kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa amefungana na Mkorea Kusini wa Tottenham, Son Heung-Min wote wakiwa na mabao 23. Heung-Min alikuwa moto akifunga mabao mawili Tottenham ikiibugiza Norwich mabao 5-0.
Kwa ushindi huo, Tottenham ilifanikiwa kushika nafasi ya nne ikiwa na pointi 71 na kuwaacha mahasimu wao wa London, Arsenal wakiwa wa tano na pointi 69 licha ya timu hiyo kuichapa Everton mabao 5-1. Arsenal na Tottenham zilikuwa katika mchuano mkali wa kusaka nafasi ya nne ili kujikatia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mbio za kujinasua na janga la kushuka daraja, ushindi wa mabao 2-1 ambao Leeds iliupata dhidi ya Brentford uliinusuru timu hiyo katika janga hilo na kuziacha Norwich, Watford na Burnley zikishuka daraja. Burnley imemaliza ligi ikiwa na pointi 35, Watford 23 na Norwich 22.
Matokeo ya mechi zote za jana ni kama ifuatavyo…
Norwich 0-5 Tottenham
Arsenal 5-1 Everton
Brentford 1-2 Leeds
Brighton 3- 1 West Ham
Burnley 1-2 Newcastle
Chelsea 2- 1 Watford
Crystal Palace 1-0 Man Utd
Leicester 4-1 Southampton
Liverpool 3-1 Wolves
Man City 3-2 Aston Villa
