Riyadh, Saudi Arabia
Mastaa wa soka duniani, Lionel Messi wa Inter Miami FC ya Marekani na Cristiano Ronaldo wa A Nassr ya Saudi Arabia watakutana katika mechi ya Kombe la Saudi mapema mwakani.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa Inter Miami jana Jumatatu kwamba timu yao itashiriki katika michuano hiyo itakayopigwa mjini Riyadh ambapo Miami itacheza na Al Hilal Januari 29 na Februari mosi itaumana na Al Nassr.
“Mechi hizi zitatoa changamoto muhimu kwa timu zetu jambo ambalo litatufaidisha wakati tukielekea kwenye msimu mpya, tuna furaha katika kundi letu kwa kupata nafasi ya kuumana na timu za hadhi ya juu za Al Nassr na Al Hilal,” alisema mkurugenzi wa michezo wa Inter Miami, Chris Henderson.
Mechi hizo hazitokuwa mara ya kwanza kwa Ronaldo na Messi kukutana, kabla ya hapo wamewahi kukutana mara 35 kwenye klabu walizokuwa wakizichezea hapo kabla pamoja na timu zao za taifa.
Kwa mujibu wa rekodi katika mechi hizo, timu alizoziwakilisha Messi zilishinda mara 16 na Ronaldo mara 10 na sare mara tisa.
Katika mechi hizo za wafalme hao wa soka duniani, Messi ana mabao 21 na asisti 12 wakati Ronaldo ana mabao 20 na asisti moja.
Messi aliyetamba na Barcelona, majira ya kiangazi mwaka huu aliachana na klabu ya PSG na kujiunga na Inter Miami wakati Ronaldo ambaye pia amewahi kuzichezea timu kadhaa ikiwao Real Madrid aliachana na Man United Januari mwaka huu na kujiunga na Al Nassr.