Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abadallah Kibadeni ametamba akisema si rahisi kuvunja rekodi yake ya kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ kwenye mechi ya Simba na Yanga hivyo kwenye mechi ya keshokutwa wajipange sawasawa.
Kibadeni ndiye mchezaji pekee aliyewahi kufunga mabao matatu kwenye mechi ya Simba na Yanga maarufu Kariakoo Derby au Dar Derby alipofanya hivyo mwaka 1977 kwenye ushindi wa mabao 6-0.
Kuelekea mechi baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Kibadeni amesema licha ya uwepo wa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele na Jean Baleke wa Simba lakini akatamba bado si rahisi wao kufanya hivyo.
“Nashukuru Mungu kwa kunipa zawadi au tuzo ya kufanya hivyo na watu wanatambua nguvu, juhudi zangu zaidi ya miaka 40 sasa hakuna aliyefikia nilipofika mimi, kwa hiyo niseme hao waliokuwepo wanaweza kufanya vizuri lakini lazima wajipange sawasawa,” alisema Kibadeni.
“(Mayele, Baleke) ni wachezaji wazuri na wanatekeleza kazi zao, sasa wanatakiwa kufanya bora zaidi, Mimi si mtabiri ila kiufundi kila mmoja ana ubora wake, sipo karibu nao siwezi kutambua sana lakini wanaonesha zile sifa za kucheza mshambuliaji wa mwisho wanazo,” alisema Kibadeni ambaye pia amewahi kuwa kocha wa timu mbalimbali ikiwamo Simba na timu ya Taifa.
Katika ushindi wa mabao 6-0, ukiachilia mabao ya Kibadeni au King Mputa, mabao mengine mawili ya Simba yalifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’, jingine Selemani Sanga wa Yanga alijifunga wakati akipambana kuokoa krosi ya Ezekiel Greyson ‘Jujuman’.
Baleke na Mayele wote wamefunga ‘hat-trick’ msimu huu na sasa wanategemewa kuvunja rekodi hiyo katika mchezo huo ingawa kazi ni ngumu kutokana na upinzani uliopo baina ya timu hizo za Kariakoo, Dar es Salaam.