Paris, Ufaransa
Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi (pichani) amewajibu aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Neymar na aliyekuwa mkurugenzi wa michezo, Leonardo akisema kwamba PSG kwa sasa ina umoja ambao haujawahi kutokea.
Neymar hivi karibuni alisema kwamba alikuwa katika wakati mgumu akiwa PSG pamoja na mchezaji mwenzake, Lionel Messi ambao katika baadhi ya mechi walijikuta wakizomewa na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo.
Leonardo naye aliwahi kunukuliwa akiushutumu uongozi wa PSG akisema kwamba Neymar, Messi na Kylian Mbappe walikosa kuungwa mkono na kuthaminiwa ili wawe katika mazingira mazuri ya kuipa timu hiyo ushindi.
Wakati Messi na Neymar wameihama timu hiyo, Mbappe ameendelea kubaki licha ya kuwapo utata kuhusu mkataba wake na Al-Khelaifi amempongeza mchezaji huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya Ufaransa pamoja na kuwajibu Neymar na Leonardo. “Kylian Mbappe ni mchezaji wa kipekee na mtu mzuri,” alisema Al-Khelaifi.
“Na timu ya PSG haijawahi kuwa katika umoja ndani na nje ya uwanja kama ilivyo sasa, hiki ni kitu ambacho tumekiona wikiendi hii katika mechi ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Lyon, tuna kocha mzuri (Luis Enrique) na mkurugenzi wa michezo, Luis Campos, na nina furaha kwa ari mpya iliyopo katika klabu,” alisema Al-Khelaifi.
Baada ya kuwakosa Messi aliyejiunga na Inter Miami FC ya Marekani na Neymar aliyetimkia Saudi Arabia, PSG ilianza Ligi 1 nchini Ufaransa kwa sare mbili kabla ya kuanza kuibuka na ushindi.
PSG ina kibarua kigumu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa kundi moja na timu za Newcastle, AC Milan na Borussia Dortmund ingawa Al-Khelaifi anaamini watakuwa na mafanikio katika fainali hizo msimu huu.
“Mwaka huu tupo katika muelekeo mpya, hatuangalii kwa sana matokeo badala yake tunaangalia kiwango na aina ya uchezaji wetu, kama tutaendelea hivyo, matokeo yatatufuata,” alisema Al-Khelaifi.
Al-Khelaifi pia alisema kuna watu wamesahau kwamba katika misimu minne iliyopita PSG ilifikia fainali na nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.