Na mwandishi wetu
Kikosi cha Yanga kinatarajia kurejea mazoezini kesho Jumatatu kujiandaa na mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na zile za Ligi Kuu NBC.
Awali, uongozi wa timu hiyo uliwapa mapumziko ya wiki moja wachezaji wake baada ya kutolewa hatua ya robo fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa kufungwa mabao 3-1 na APR ya Rwanda.
Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison alisema leo Jumapili kuwa wanarejea kambini mapema kuhakikisha wanashinda mechi zao mbili za hatua ya makundi na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tunaanza mazoezi Jumatatu, wachezaji wote wanazo taarifa hizo na uongozi umeshafanya maandalizi yote na kocha wetu, Miguel Gamondi amesema lengo lao ni kushinda mechi zao mbili zilizobaki Ligi ya Mabingwa dhidi ya CR Belouizdad na Al Ahly ili kufuzu robo fainali,” alisema Walter.
Meneja huyo alisema Gamondi amewataka wachezaji wote ambao hawako kwenye majukumu ya timu zao za taifa katika michuano ya Afcon inayoendelea Ivory Coast, kuripoti mazoezini kesho kambini kwao Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam.
Katika msimamo wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa, Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano sawa na Al Ahly lakini vinara hao wapo nyuma kwa mchezo mmoja.