Na mwandishi wetu
Yanga imefuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (FA) baada ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la Azam Complex na kutawaliwa na ushindani mkali.
Kwa ushindi huo uliopatikana Jumamosi hii, Yanga sasa inasubiri kuivaa Singida Big katika nusu fainali ya michuano hiyo wakati Simba itaumana na Azam katika nusu fainali nyingine.
Alikuwa ni Fiston Mayele aliyepeleka kilio Geita katika dakika ya 58 baada ya kuinasa pasi safi ya Tuisila Kisinda na kuipatia Yanga bao hilo pekee katika mchezo huo.
Dakika moja kabla ya kuingia bao hilo, Geita ilipata pigo baada ya mchezaji wake, Geofrey Manyasi kutolewa uwanjani kwa kupewa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu Mayele.
Upambanaji wa Geita katika mechi hiyo ulijidhihirisha hasa kipindi cha kwanza na pengine hiyo ikawa sababu ya benchi la ufundi Yanga kumuingiza Mayele ambaye ndiye aliyeokoa jahazi. Mayele aliingia akichukua nafasi ya Clement Mzize.
Geita licha ya kucheza pungufu uwanjani bado hawakuonekana kutetereka na ingawa walishindwa kusawazisha bao hilo upambanaji wa wachezaji wa timu hiyo uliwapa wakati mgumu mastaa wa Yanga kutumia upungufu wa wachezaji wa Geita kuongeza bao la pili.
Wachezaji wa Yanga akiwamo winga Benard Morrison ambaye alionekana mara ya kwanza katika mechi hiyo baada ya kukosekana kwa muda mrefu, walikumbana na ubabe wa wachezaji wa Geita hali iliyomfanya mwamuzi mara kadhaa kuwaonya kwa mdomo na wakati mwingine kutoa kadi ya njano.
Geita inakuwa imepoteza kwa mara ya pili mfululizo mechi na Yanga katika michuano hiyo kwenye robo fainali, Aprili mwaka jana ilipoteza kwa penalti 7-6 baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida.
Soka Yanga yatua nusu fainali FA
Yanga yatua nusu fainali FA
Read also