Na mwandishi wetu, Tanga
Yanga imetinga fainali ya michuano ya Ngao ya Jamii kwa kuichapa Azam FC mabao 2-0 yaliyofungwa na Stephanie Aziz Ki na Clement Mzize katika mechi iliyopigwa leo Jumatano Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Aziz Ki aliyeingia akitokea benchi, alifunga bao lake dakika ya 84 baada ya kuonesha uwezo binafsi kwa ‘kuwafinya’ mabeki wawili wa Azam kabla ya kufumua shuti la mguu wa kushoto lililomshinda kipa, Zubeir Masoud Foba na kujaa wavuni.
Dakika nne baadaye, Mzize alikamilisha idadi ya mabao ya Yanga akiyatumia makosa ya mabeki wa Azam walioshindwa kuumiliki mpira uliokuwa katika himaya yao na kufumua shuti lililojaa wavuni.
Mechi ya leo ilionekana kuwa ngumu kwa timu zote hasa katika kipindi cha kwanza huku wachezaji wa pande zote wakichezeana rafu za hapa na pale zilizomlazimu mwamuzi kutoa kadi za njano na wakati mwingine kuwaonya kwa maneno.
Katika kipindi hicho nyota wa zamani wa Yanga, Fei Toto alichezewa rafu mara mbili hadi kulazimika kumlaumu mwamuzi akimtaka atoe hadi hasa pale alipochezewa rafu na Mudathir Yahya hadi kuanguka chini.
Yanga hata hivyo walijitahidi kutengeneza nafasi nyingi ambazo walishindwa kuzitumia, mfano katika dakika ya 22, Maxi Nzengeli alimzidi ujanja kipa wa Azam aliyekuwa ametoka golini na kufumua shuti la kima cha mbuzi lakini beki wa Azam Edward Manyama aliuwahi mpira huo na kuutoa kwa kichwa.
Dakika ya 78, Mudathir Yahya alimuunganishia pasi ya kichwa Mzize ambaye alifumua shuti lililogonga mwamba na kuwafanya mashabiki wa Yanga wabaki wameshangaa wasiamini kilichotokea.
Kwa matokeo hayo, Yanga sasa inamsubiri mshindi wa mechi kati ya Singida Fountain Gate na Simba itakayopigwa kesho Alhamisi ili ikutane nayo Jumapili katika mechi itakayotoa mshindi wa michuano.
Michuano ya Ngao ya Jamii kwa mara ya kwanza msimu huu imeshirikisha timu nne badala ya mbili zilizozoeleka katika michuano iliyopita, ni timu ambazo zimeshika nafasi ya kwanza hadi ya nne kwenye Ligi Kuu NBC ambazo zinacheza kwa mtoano.
Soka Aziz Ki, Mzize wainyoosha Azam
Aziz Ki, Mzize wainyoosha Azam
Read also