Madrid, Hispania
Jose Mourinho au Speacial One anadaiwa kusaini mkataba wa miaka mitatu na klabu ya Real Madrid ingawa atatangazwa rasmi baada ya uchaguzi wa rais wa klabu hiyo utakaofanyika Juni 7, 2026.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Mourinho kuinoa timu hiyo ingawa uhalali wa mkataba wake upo njia panda na kila kitu kitajulikana rasmi baada ya rais wa sasa, Florentino Perez kuchaguliwa tena katika nafasi hiyo.
Mourinho, 63, amekuwa akihusishwa katika nafasi hiyo mara kadhaa tangu kuondoka kwa Xabi Alonso Januari mwaka huu na nafasi yake kukabidhiwa kocha wa muda, Alvaro Arbeloa.
Kwa kukubali kuinoa Real Madrid, Mourinho anaachana na klabu ya Benfica ambayo alianza kuinoa Septemba mwaka jana na ameiwezesha kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Ureno maarufu Primera Liga msimu huu.
Akiwa na Real Madrid mara ya kwanza kati ya mwaka 2010 hadi 2013, kocha huyo kutoka Ureno aliiwezesha timu hiyo kutwaa mataji ya La Liga, Copa del Rey na Spanish Super Cup.
Mourinho pia amewahi kuzinoa timu za FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Tottenham, Man United, AS Roma na Fenerbahce.
Msimu huu wa 2025-26 na msimu uliopita imekuwa migumu kwa Real Madrid ikimaliza bila taji lolote na msimu huu imeuaga kwa kichapo cha mabao 2-0 mbele ya mahasimu wao Barcelona katika El Clasico.
Perez, 79, anaamini Mourinho ana uwezo wa kurudisha heshima Real Madrid ingawa bado ana kazi ya kuchuana katika kiti cha urais wa klabu hiyo na Enrique Riquelme, bilionea aliyewekeza katika nishati jadidifu.
Tangu mwaka 2009, Perez amekuwa Real Madrid akikosa mpinzani tishio katika kiti cha urais na kabla ya hapo aliiongoza klabu hiyo kati ya mwaka 2000 na 2006, safari hii licha ya kupewa nafasi kubwa ya kushinda urais, ujasiri wa Riquelme unaacha maswali mengi.
Kimataifa Mourinho asaini mkataba Real Madrid
Mourinho asaini mkataba Real Madrid
Read also
