Na mwandishi wetu
Uongozi wa Klabu ya Simba umekamilisha utambulisho wa watendaji wake wa benchi la ufundi leo Alhamisi kwa kutangaza cheo kipya walichomuajiri Mkenya, Mikael Igendia kuwa meneja wa timu na mkuu wa sayansi ya michezo.
Igendia, 36, aliyesaini mkataba wa miaka miwili, ametua kurithi mikoba ya Patrick Rweyemamu ambaye amekuwa mkuu wa programu za soka la vijana ambaye awali alikuwa meneja wa timu pekee.
Mtaalamu huyo anayemudu kwa ufanisi pia masuala ya utimamu wa mwili, amewahi kufanya kazi na Gor Mahia ya Kenya, timu ya Taifa ya Kenya na Taifa Stars aliyokuwa akiitumikia kabla ya kutua kwa Wekundu hao.
Utambulisho huo unakuwa wa tatu kwa Simba baada ya awali saa saba mchana kumtambulisha Daniel Cadena, 45 kuwa kocha wao mpya wa makipa kwa mkataba wa miaka miwili kabla ya saa tatu baadaye kumtaja Corneille Hategekimana kuwa kocha mpya wa viungo kwa mkataba wa miaka miwili pia.
Cadena ambaye ni kocha raia wa Hispania mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), ametua Simba baada ya kumaliza mkataba wake Azam FC alikohudumu kwa msimu mmoja.
Cadena amerithi nafasi ya Chlouha Zakaria raia wa Morocco aliyeachana na timu hiyo takriban wiki nne zilizopita.
Naye Hategekimana, 47 raia wa Rwanda amechukua kandarasi hiyo akitokea AS Kigali ya nchini kwao akiwa amefuzu mafunzo ya kozi mbalimbali za viungo kwa wachezaji, diploma ya uongozi wa michezo, mkufunzi wa viwango (GPS) kwa wachezaji, kozi ya juu ya viungo inayotolewa na Fifa, amechukua nafasi ya Kelvin Mandla.
Wataalamu hao wanatarajia kukutana na kocha mkuu wa benchi la timu hiyo, Robert Oliveira ‘Robertinho’ anayetarajia kujiunga na timu hiyo hivi karibuni akitokea mapumzikoni nyumbani kwao Brazil kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa 2023-24.