London, England
Arsenal sasa italazimika kukaza buti ili kuingia vitani na Man City katika kuiwania saini ya kiungo wa West Ham, Declan Rice (pichani) baada ya Man City nao kuwasilisha ofa ya kumtaka mchezaji huyo.
Kwa kipindi kirefu Arsenal imekuwa ikitajwa kumtaka Rice ambaye hivi karibuni aliweka rekodi kwa kuiwezesha West Ham kutwaa taji la Europa Conference Ligi huku akiwa mmoja wa wachezaji ambao soka lao lilivutia wengi.
Tayari ofa za Arsenal zimekataliwa mara mbili, ya mwisho ilikuwa ya Pauni 90 milioni iliyokataliwa juzi Jumanne lakini habari za leo Alhamisi kuhusu City kumtaka mchezaji huyo zinaifanya Arsenal kupata mpinzani wa kwanza katika mpango huo.
Habari za ndani zinadai kwamba City walikuwa wakisubiri kujua hatma ya kiungo na nahodha wao Ilkay Gundogan kama angebaki katika klabu hiyo.
Gundogan hata hivyo amekataa kusaini mkataba mpya na City na kuamua kujiunga na Barcelona, kocha wa Man City, Pep Guardiola sasa anaamini Rice ambaye pia anaichezea timu ya Taifa ya England ndiye mtu sahihi wa kuchukua nafasi ya Gundogan.
Uamuzi wa Man City umekuja wakati ambao Arsenal wanajiandaa kuja na ofa nyingine kwa mara ya tatu huku kukiwa na habari kwamba West Ham wanaamini thamani ya Rice ni zaidi ya Pauni 100 milioni.
Na ingawa Arsenal wamekuwa wakijiamini kuwa na uwezo wa kumpata mchezaji huyo lakini kwa sasa itabidi ijulikane kwanza ofa ambayo Man City wamejiandaa kuiweka mezani.
Kwa upande wa Rice ambaye ana mkataba na West Ham unaofikia ukomo mwaka 2024, amewahi kunukuliwa akisema kwamba anataka kwenda kusaka changamoto mpya nje ya klabu hiyo.
Kimataifa Rice aziingiza vitani Arsenal, Man City
Rice aziingiza vitani Arsenal, Man City
Read also