Eindhoven, Uholanzi
Kipa wa Sevilla, Marko Dmitrovic jana Alhamisi usiku alivamiwa uwanjani na shabiki wa PSV Eindhoven ambaye alimrushia ngumi na kipa huyo kupambana naye kabla ya wana usalama kuingilia kati.
Tukio hilo lilitokea wakati timu hizo zikiumana katika mechi ya Europa Ligi, ndipo shabiki huyo wa timu mwenyeji alipomvamia kipa ambaye hata hivyo aliendelea na mchezo licha ya timu yake kufungwa 2-0.
Kwa matokeo hayo, Sevilla imefuzu hatua ya 16 bora ya michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 baada ya awali kushinda mechi ya kwanza kwa mabao 3-0.
Dmitrovic ambaye pia aliwahi kuidakia Charton Athletic baada ya tukio hilo aliwaambia waandishi wa habari kwamba halikuwa jambo zuri katika soka na anaamini hatua zitachukuliwa.
“Haijawahi kuwa vizuri kuona mchezo wa soka unakuwa na mambo haya, haikutakiwa kamwe kutokea hali hii na kuanzia sasa natarajia adhabu zitatolewa kwa matukio haya,” alisema Dmitrovic.
“Alikuja akitokea kwa nyuma, akanisukuma, nadhani alikuwa na hasira na matokeo, alikuwa akijaribu kunipiga lakini nilifanikiwa kumshika na kuwasubiri watu wa usalama wafike.”
Kocha wa Sevilla, Jorge Sampaoli alielezea kusikitishwa na tukio hilo na kuongeza kwamba inaogopesha kuona mambo ya aina hiyo yanajitokeza na ni lazima wanaofanya mambo haya waache.
Shabiki huyo ambaye picha zimemuonyesha akikunja ngumi kwa nia ya kupigana lakini wakati wote kipa alitumia muda mwingi kumdhibiti hadi wana usalama walipofika na kumuweka chini ya ulinzi.
Hata alipoanguka chini bado shabiki huyo alikuwa akijitahidi kupambana na kipa kiasi cha kumshika jezi sehemu ya kifuani lakini kilichoonekana ni kwamba Dmitrovic hakuwa tayari kujibu mapigo.
Tukio la kuvamiwa kwa kipa huyo linafanana na lile lililomkuta kipa wa Arsenal, Aaron Ramsdale ambaye katika mechi dhidi ya mahasimu wao Tottenham iliyochezwa Janauri 15 alivamiwa na kupigwa teke na shabiki anayeaminika kuwa wa Tottenham.
Shabiki huyo ambaye inadhaniwa alikuwa amelewa pia inadhaniwa alichukizwa na matokeo ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata Arsenal, baadaye alikamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo alikiri kosa.