London, England
Nyota wa Man United, Luke Shaw amesema kwamba nyota mwenzake wa timu hiyo na timu ya Taifa ya England, Harry Maguire anakutana na shutuma ambazo hajawahi kukutana nazo kwenye soka.
Maguire, beki wa kati wa England alifanya makosa yaliyoiwezesha Ujerumani kupata mabao mawili kati ya matatu ambayo timu hiyo iliyapata katika mechi ya Uefa Nations Ligi iliyochezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Wembley na timu hizo kutoka sare ya 3-3.
Hatua ya kocha Gareth Southgate kumpanga Maguire katika mechi hiyo imekuwa ikijadiliwa hasa baada ya mchezaji huyo kusugua benchi katika kikosi cha Man United. “Harry ni mchezaji mzuri, ana tabia za kipekee, amekuwa akishutumiwa sana, pengine sijawahi kuona hapo kabla mchezaji mwingine yeyote akifanyiwa hivyo,” alisema Shaw.
“Hajawahi kuwa mtu wa kujificha wakati wote ni yule yule, kuna watu ambao wanaweza kujificha, hawataki kuonekana hadharani, lakini yeye ameendelea kujitoa hadharani, hiyo inaonyesha alivyo imara na mwenye tabia sahihi,” alisema Shaw.
“Kila mtu anafahamu kwamba ni mchezaji mzuri, wakati huu anaweza kukosa hali ya kujiamini kwa sababu anajiona kama dunia yote inampiga vita, ni jambo gumu kwake lakini sisi wachezaji pamoja na maofisa wa timu tuko pamoja naye kwa sababu ni mchezaji muhimu, inaonyesha Gareth anavyomuamini kwa sababu amekuwa akimpanga na tuangalie alichofanya kwenye Euro,” alisisitiza Shaw.
Maguire amekuwa katika wakati mgumu kwenye kikosi cha England na Man United, Machi mwaka huu alizomewa na mashabiki katika mechi ya kirafiki ya England dhidi ya Ivory Coast.
Mwezi uliofuata polisi walilazimika kufanya ukaguzi katika nyumba yake baada ya kupata taarifa za vitisho vya kutegewa bomu, pia akiwa Man United kwenye ziara za kabla ya msimu alijikuta akizomewa na mashabiki nchini Australia.
Hadi sasa katika Ligi Kuu England amecheza mechi tatu tu lakini pamoja na yote hayo, bado kocha wa timu ya England anamuamini lakini imani hiyo huenda ikamshinda kocha huyo ambaye aliwahi kusema kwamba Maguire anahitaji kujihakikishia namba katika klabu ili awemo kwenye kikosi cha England kitakachokwenda Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Kimataifa Wanaomsakama Maguire wamkera Luke Shaw
Wanaomsakama Maguire wamkera Luke Shaw
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
