Na mwandishi wetu
Yanga kuchukua taji la Ligi Kuu ya NBC msimu huu ni suala la muda tu, ni vigumu kuwazuia, je muda huo ni Jumatano hii timu hiyo itakapoumana na Coastal Union? Au Coastal itakubali kufanywa daraja?
Timu hizo zinaumana Jumatano hii katika mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu na wa kuvutia kutokana na malengo ya timu zote mbili kuelekea mechi za mwisho za kufunga pazia la ligi hiyo msimu huu.
Yanga ikipata ushindi kwenye mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam itakuwa imeifanya Coastal kama daraja, itafikisha pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine na kutangaza ubingwa wake wa kwanza baada ya miaka minne lakini iwapo itashindwa italazimika kusubiri mechi mojawapo kati ya tatu zitakazobakia ili kutangaza ubingwa.
Ushindi huo muhimu kwa Yanga mbali na kuwawezesha kunyanyua ndoo ya ligi hiyo lakini pia utakuwa ni mwendelezo wa timu hiyo kutopoteza mechi mpaka sasa, ikiwa imeshinda mechi 19 na sare saba.
Azma hiyo ya Yanga inaweza kuwa ngumu kutimia kutokana na Coastal yenyewe pia kuhitaji ushindi ili kujitengenezea mazingira rafiki ya kumaliza kwenye nafasi nne za juu ili ishiriki michuano ya klabu Afrika msimu ujao.
Coastal yenye maskani yake Tanga mpaka sasa inashikilia nafasi ya sita kwa pointi 34 ikizidiwa pointi tatu na Azam na Namungo zinazoshikilia nafasi ya tano na ya nne huku Geita iking’ang’ania kwenye nafasi ya tatu kwa pointi 39.
Mbali na hilo mechi hiyo pia inatarajia kutoa mbabe baina ya timu hizo baada ya mechi mbili za mwisho kila timu kuibuka na ushindi wa mechi moja. Coastal iliibamiza Yanga mabao 2-1 kabla ya Yanga nao kuitandika timu hiyo mabao 2-0.
Kingine, Coastal itaingia dimbani ikiwa na ushindi wa mechi nne na sare moja kwenye mechi zake tano za mwisho za ligi na ni wazi watataka kuiendeleza rekodi hiyo kwa ushindi wakati Yanga katika idadi ya mechi hizo imeshinda mbili na kutoa sare tatu.
Kocha Mkuu wa Coastal, Juma Mgunda anaamini mechi hiyo ni ngumu kutokana na ubora wa kikosi watakachokutana nacho, pia azma ya ubingwa walionayo wapinzani wao huku wao nao wakitaka kutimiza malengo waliyonayo kwa kupata ushindi.
“Mchezo ni mgumu, tunakutana na timu inayoongoza ligi, ina wachezaji wazuri na wazoefu, wanataka ubingwa pia kwa hiyo wao wana malengo yao na sisi pia tuna malengo yetu kuelekea mechi hiyo hiyo.
“Ndiyo maana nasisitiza mechi hii si rahisi hata kidogo maana na sisi pia tunahitaji kufanya vizuri, tunataka kusogea juu kutimiza tunachokitaka msimu huu, ndiyo maana naendelea kusema bila wasiwasi, mechi hii ni ngumu mno,” alisema Mgunda.
Wakati Mgunda, mchezaji wa zamani wa Coastal akiyasema hayo, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema: “Kwanza hii mechi ni ngumu kwa sababu hawa Coastal tutakutana nao mara tatu, hivyo matokeo ya mechi hii yatatoa taswira ya mechi zijazo.
“Kwa kulitambua hilo nimekuwa nikizungumza na vijana wangu kila wakati kuwakumbusha umuhimu wa mechi hii kutokana na mambo mbalimbali ambayo yanafahamika kwa ajili ya kutimiza malengo yetu mapema,” alisema Nabi.
Nabi ameweka wazi pia kuwakosa wachezaji wake ambao ni kipa Djigui Diarra, Kibwana Shomari na Bakari Mwamnyeto. Diarra ametajwa kuchelewa kujiunga na wenzake akitokea kwenye majukumu ya timu yake ya taifa.
Mwamnyeto pia ameelezwa kwamba aliumia wakati akiwa kwenye majukumu ya Taifa Stars wakati Shomari ni kutokana na adhabu ya kadi tatu za njano alizooneshwa.
Timu hizo zikimalizana mechi hii, zitakutana tena Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha mnamo Julai 2, mwaka huu kwa ajili ya fainali ya Kombe la Azam (ASFC) huku zikitarajia kukutana tena kwenye mechi ya Ngao ya Jamii msimu ujao wa 2022-23.
Mwisho.
