Arlington, Texas
Zama za mwanasoka mahiri duniani, Cristiano Ronaldo kwenye timu ya taifa ya Ureno zimefika mwisho baada ya timu hiyo kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 na yeye kutoka mikono mitupu kwenye michuano hiyo.
Ureno imetolewa na Hispania kwa kuchapwa bao 1-0 katika mechi ya hatua ya mtoano (16 bora) iliyopigwa mjini Dallas, Jumatatu Julai 6, 2026 huku Ronaldo akiaga na kutangaza mapema kuwa hizi ni fainali zake za mwisho.
Bao hilo pekee la dakika ya 46 lililofungwa na Mikel Merino limemfanya Ronaldo kuungana na nyota wa Brazil, Neymar Jr ambaye naye ameachana na timu hiyo huku wote wakitoka uwanjani na vilio baada ya timu zao kutolewa.
Kutolewa kwa Ureno kunamfanya Ronaldo aondoke katika timu hiyo akiwa hajawahi kubeba Kombe la Dunia licha ya mafanikio makubwa aliyopata katika soka ikiwamo kutwaa tuzo ya Ballon d’Or mara tano.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 41 mbali na Ballon d’Or na Kombe la Ulaya alilobeba mwaka 2016 (Euro 2016) ana rekodi ya kubeba mataji ya ligi mbalimbali kubwa Ulaya ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano.
Mchezaji huyo anaachana na timu ya Ureno akiwa ameiwakilisha kwenye fainali sita za Kombe la Dunia na mafanikio yake katika michuano hiyo ni mwaka 2006 katika fainali zake za kwanza ambapo Ureno ilifikia hatua ya nusu fainali.
Ushiriki wa Ronaldo katika fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazofanyika katika mataifa ya Canada, Marekani na Mexico ulipingwa na baadhi ya wachambuzi kwa hoja kwamba mchezaji huyo amefikia mwisho.
Kocha wa Ureno, Roberto Martinez amekuwa na mtazamo tofauti na wachambuzi hao kwa kumtetea Ronaldo hata baada ya Ureno kutolewa na rekodi kuonesha kwamba mchezaji huyo hakuwa na mchango wa maana kwenye timu.
Kimataifa Ronaldo astaafu timu ya taifa
Ronaldo astaafu timu ya taifa
Read also
