Na mwandishi wetu
Uongozi wa Simba leo Jumatano umemtangaza Selemani Matola kuwa kocha mkuu wa timu za vijana za klabu hiyo na Patrick Rweyemamu kuwa Mkuu wa Programu za Vijana.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema hakuna kocha bora wa kumpa majukumu ya soka la vijana kama Matola ambaye atakuwa akisimamia timu za umri chini ya miaka 17 hadi 20.
“Ukichunguza timu kubwa za Afrika wana timu za vijana imara ambazo baadae wanaingia kwenye timu ya wakubwa. Leo tunatoa taarifa ya kuboresha timu zetu za vijana.
“Matola atakuwa kocha mkuu wakati mkuu wa programu za vijana atakuwa Patrick Rweyemamu, hadi ninapoongea sasa, Rweyemamu bado ni meneja wa timu ya wakubwa lakini pia haya majukumu tumempa yeye. Katika siku chache zijazo tutasema tunafanya nini ili kuboresha timu zetu,” alisema Kajula.
Naye Matola ambaye amewahi kuwa kocha msaidizi Simba alisema: “Kwanza niipongeze bodi na uongozi kwa kuona hili, kwetu sisi si jambo geni. Tulishafanya na tulifanikiwa sana. Naamini sasa tutazalisha vitu vizuri zaidi ikiwezekana zaidi ya ile ya mwanzoni. Sitowaangusha wapenzi wa Simba, nitafanya kile wanachohitaji kwenye maendeleo ya vijana.”
Naye Rweyemamu alisema: “Mpira hauwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji kwa vijana. Kuanzia 2008 hadi 2015 tumetoa wachezaji takribani 250. Hakuna timu za ligi kuu hadi madaraja ya chini hawajawahi kukosa wachezaji ambao wamepita kwenye timu ya vijana ya Simba.
“Tunatafuta wachezaji wenye vipaji, wenye uwezo, tunatengeneza ajira na tunapunguza mchakato wa usajili sababu kutafuta kitu ambacho hujawekeza kina gharama yake na kuna kizazi kinapotea kwenye mpira hivyo lazima tuandae kizazi kipya ambacho kitasaidia Simba na taifa kwa ujumla.”
