Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri amesema matokeo bora wanayoyapata sasa ni kutokana na kiwango bora cha kila mchezaji wa timu hiyo na ushirikiano mkubwa wanaopeana sasa.
Simba ilipata matokeo ya ushindi ugenini wa mabao 3-1 mjini Luanda, Angola dhidi ya Primeiro de Agosto Jumapili iliyopita huku wakionesha kiwango kikubwa kwenye mechi hiyo ya awamu ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Phiri ambaye alifunga bao moja katika ushindi huo alisema anashukuru kwa matokeo hayo kwani yanapatikana kutokana na ufanisi wao mkubwa unaochangiwa na benchi la ufundi kwenye kupanga kikosi bora katika kila mchezo kwa kadri inavyowezekana.
“Nadhani tulifanya vizuri kama timu ndiyo maana tulipata ushindi ule, kama wachezaji wasingekuwa bora nadhani matokeo yangekuwa tofauti, lakini kwa kiwango bora cha kila mchezaji na mawasiliano mazuri tuliyokuwa nayo nadhani yalisababisha tushinde mchezo ule.
“Benchi la ufundi pia linafanya kazi yake kwani tuna michezo mingi ndIyo maana makocha wamekuwa na uamuzi wa kubadili wachezaji kulingana na mechi na nafikiri hiyo ni sababu sababu ya kutupa ushindi,” alisema Phiri.
Mshambuliaji huyo raia wa Zambia mpaka sasa amefunga mabao matano kwenye mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika. Alifunga bao moja walipokuwa ugenini dhidi ya Nyassa Big Bullets waliposhinda mabao 2-0 kabla ya kufunga mabao mawili walipoitungua timu hiyo nyumbani kwa mabao 2-0.
Simba ambayo imerejea nchini jana asubuhi, leo imeanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wake wa marudiano na Agosto utakaopigwa Oktoba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ikihitaji sare au ushindi ili kutinga hatua ya makundi na kama itapoteza basi isiruhusu kufungwa mabao 3-0.
Soka Phiri ataja siri ya ushindi Simba
Phiri ataja siri ya ushindi Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
