Manchester, England
Manchester City leo imethibitisha kumsajili beki, Sergio Gomez kwa ada ya Pauni 11 milioni na mkataba wa miaka minne.
Gomez ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Hispania ya vijana chini ya miaka 21 ametua, Man City akitokea Anderlecht ya Ubelgiji na amewahi kuwa kwenye akademi ya Barcelona kabla ya kwenda Anderlecht ambapo amekuwa chini ya nahodha wa zamani wa Man City, Vincent Kompany.
“Nina furaha kwa kupewa fursa na klabu ya Manchester City, na nitajaribu kujitoa katika ubora wangu uwanjani, kwa pamoja tunaweza kufanikisha mambo makubwa,” alisema Gomez na kumpongeza Kompany kwa mchango mkubwa alioutoa katika kukuza kipaji chake cha soka na hivyo anajivunia kufanya naye kazi tangu siku ya kwanza.
“Nilizowea kuiangalia Man City kwenye televisheni wakati nikiwa mdogo, na wakati huo Kompany alikuwa nahodha, alikuwa ni mfano wa kuigwa kwa kila mtu, kwangu ni heshima kubwa kufanya naye kazi na namshukuru kwa kila kitu kilichotokea msimu uliopita katika klabu ya Anderlecht,” alisema.
“Nilizungumza naye siku chache zilizopita, nilimwambia kuhusu fursa ya kwenda Manchester City na akaniambia amefurahishwa na mimi kwa hatua kubwa niliyopiga katika maisha yangu ya soka,” aliongeza Gomez.
Kwa muda mrefu Man City imekuwa ikisaka beki wa kushoto tangu kuikosa saini ya Marc Cucurella aliyesajiliwa na Chelsea wakati huo ikiwa imeondokewa na Oleksandr Zinchenko na kuiacha klabu hiyo ikiwa imebakiwa na mzoefu pekee Joao Cancelo pamoja na kinda Josh Wilson.
Tayari kocha wa Man City, Pep Guardiola ameshasema kwamba Gomez hatouzwa kwa mkopo wakati mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Txiki Begiristain alimsifia mchezaji huyo akisema, “maendeleo ya Sergio katika misimu ya hivi karibuni yamekuwa kivutio, ni beki aliyekamilika na anayetarajiwa kufanya mambo makubwa.”
Kimataifa Gomez amwaga wino Man City
Gomez amwaga wino Man City
Read also