Buenos Aires, Argentina
Straika wa zamani wa Man United na Man City, Carlos Tevez hatimaye ameamua kustaafu rasmi soka akiwa na umri wa miaka 38.
Tevez amechukua uamuzi huo ikiwa ni takriban miaka minne imepita tangu aamue kurudi nyumbani kwao Argentina na kujiunga na klabu yake ya utotoni ya Boca Juniors ambayo pia aliachana nayo Juni mwaka jana. Alijiunga na Boca akitokea China alikokuwa akiichezea klabu ya Shanghai Shenhua.
Kwa mashabiki wa soka, Tevez anakumbukwa kwa mengi lakini mojawapo ni juhudi zake za kuiokoa West Ham isishuke daraja katika msimu wa 2006/07 hapo hapo anakumbukwa kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuihama Man United na kujiunga na majirani na mahasimu wao Man City.
Akizungumzia uamuzi wa kustaafu, Tevez alisema pamoja na mambo mengine umechangiwa na kifo cha baba yake kilichotokea mwaka jana. “Nimestaafu soka kwa sababu nimempoteza shabiki wangu namba moja, nimepata ofa nyingi zikiwamo za Marekani lakini hapo ndipo nilipofikia, nimejitoa kwa kila kitu.”
Tevez alisema kwamba kwa mwaka jana kucheza kwake soka kulikuwa na ugumu kwani baba yake mzee Segundo Tevez akiwa na miaka 58 alifariki Februari 2021 kutokana na maradhi ya corona.
Akiwa na timu ya Taifa ya Argentina, Tevez ameichezea timu hiyo mara 75 lakini pia aliwahi kushinda medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya Athens mwaka 2004.
Uamuzi wake wa kuihama Man United mwaka 2009 ulionekana kuwashitua wengi hasa kwa kuwa alikuwa akihamia kwa mahasimu wao Man City baada ya kupata mafanikio Man United akiwa na mataji mawili ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kimataifa Carlos Tevez astaafu soka
Carlos Tevez astaafu soka
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
