Liverpool, England
Klabu ya Liverpool imekataa ofa ya Pauni milioni 150 kutoka klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia inayomtaka mshambuliaji wake, Mohamed Salah (pichani) na kusisitiza kuwa mshambuliaji huyo hauzwi.
Salah alijiunga na Liverpool, mwaka 2017 akitokea Roma ya Italia, mwaka jana alisaini mkataba mpya na Liverpool wa miaka mitatu lakini katika siku za karibuni amekuwa akitakiwa na Al-Ittihad.
Wiki iliyopita, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alisema kwamba Salah amejitoa kwa asilimia 100 kwa ajili ya klabu hiyo ya Anfield na jana Ijumaa kocha huyo alisisitiza kwa mara nyingine akisema kwmaba mchezaji huyo hauzwi.
“Msimamo unabaki vile vile, hakika hakuna shaka katika hilo, hivyo ndivyo ilivyo na hakuna zaidi ya hilo,” alisema Klopp.
Na ingawa hadi jana Ijumaa usiku ambayo ilikuwa siku ya mwisho kwa usajili Liverpool ilikuwa na hofu ya kumpoteza mshambuliaji huyo ingawa hata sasa lolote linaweza kutokea kwa kuwa kipindi cha usajili kwa ligi ya Saudi Arabia kinafikia ukomo Septemba 7.
Katika mechi tatu alizocheza tangu kuanza kwa msimu mpya wa 2023-24, Salah tayari ameifungia Liverpool bao moja na ana asisti mbili huku akiwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa timu hiyo.
“Mohamed anabaki kuwa mchezaji wa Liverpool, kama tungekuwa na mpango wa kuondoka Liverpool mwaka huu tusingesaini mkataba mpya mwaka jana,” alisema Ramy Abbas Issa ambaye ni wakala wa Salah.