London, England
Kocha wa muda wa Chelsea, Frank Lampard amewalaumu wachezaji wake kwa kutokuwa wapambanaji na sasa ana kazi ya kuweka mambo sawa kabla ya mechi ya Jumanne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Lampard alitoa kauli hiyo baada ya Chelsea ikiwa nyumbani kufungwa mabao 2-1 na Brighton na kubaki nafasi ya 11 kwenye Ligi Kuu England huku ikipoteza matumaini ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
“Nimekatishwa tamaa katika kila eneo, timu nzuri ilishinda na ingeweza kushinda zaidi, walicheza kitimu, wanacheza kwa pamoja kwa muda mrefu, tuwape heshima yao,” alisema Lampard.
“Lakini kwa upande wetu haitoshi, mambo ya msingi katika soka, kupambana, kukimbia na mambo kama hayo tulikuwa na upungufu, ni lazima tutoke katika hilo kwa haraka sana,” alisema.
“Tuna mechi kubwa Jumanne, hatuhitaji kuwa nyuma, badala yake tuwe profesheno ni lazima tuelewe ni kwa nini leo (jana Jumamosi) tumefanya tulichofanya na hakikuwa kizuri kwa upande wetu,” aliongeza.
Chelsea imepoteza mechi zote tatu tangu Lampard akabidhiwe jukumu la kuinoa timu hiyo kutoka kwa Graham Potter lakini kocha huyo amedai kwamba kiwango cha timu hiyo katika mechi na Brighton ndicho kikilichomkatisha tamaa zaidi.