Na mwandishi wetu
Bondia wa ngumi za kulipwa, Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ amesema mabondia wengi wa Tanzania wanashindwa kufanya vizuri katika mechi za kimataifa kutokana na kukosa maandalizi mazuri na wengine kukabiliwa na ukata wa pesa.
Amesema mara kadhaa wanapoenda katika mechi za kimataifa kwanza huwa wanashtukizwa na huchukua maamuzi ya kupigana bila hata ya kupata watu wa kuwaandaa kimazoezi kwa sababu tu ya kupata pesa na kingine wanajua hata kama watashindwa hakuna wa kuwacheka na kuwakosoa.
“Mabondia wengi tunapitia kwenye mazingira magumu hatuna mazoezi ya kutosha na kingine tunapoenda katika mechi za kimataifa hatushindi kwa sababu unakuta hatujajiandaa, tunachofuata kule ni fedha tu,” alisema bondia huyo wa uzito wa kati.
Pamoja na hayo, Dullah pia ametoa wito kwa makampuni na wawezeshaji kujitokeza kuwapa ubalozi na vitu vingine kama hivyo vitakavyowawezesha kupata pesa na hata upatikanaji wa bima za afya kwa mabondia ili nao waweze kukidhi matakwa ya mchezo huo na kuwa kwenye ushindani unaostahili.
“Kuna muda unafikia huna hata senti, ukiangalia mazingira unayoishi ni magumu na mabondia hatuna hata bima za afya, tunaomba makampuni yawekeze kwetu, tuwatangazie bidhaa zao ili na sisi tupate fedha za kutusaidia kuendeleza maisha yetu ya kila siku na angalau tuweze kujiandaa vizuri kimchezo tukiwa hatuna msongo wa mawazo mengine ya kimaisha,” alisema.
Aliongeza kuwa changamoto nyingine iliyopo ni kwamba viongozi walionao katika tasnia ya ngumi bado hawajawa makini kwani wako kwenye makundi na wanapigana majungu badala ya kujadili nini cha kufanya kuusogeza mbele mchezo huo.
Ngumi Dulla Mbabe: Tatizo maandalizi, ukata
Dulla Mbabe: Tatizo maandalizi, ukata
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
