Manchester, England
Wakati habari za kufutwa kazi mwishoni mwa msimu huu zikiwa zimepamba moto, kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema kwamba hasumbuliwi hata kidogo na jambo hilo.
Kipigo cha mabao 4-0 ambacho timu hiyo ilikipata Jumatatu iliyopita dhidi ya Crystal Palace kimezidi kuiweka pabaya Man United ambayo sasa inashika nafasi ya nane katika Ligi Kuu England (EPL) na Jumapili itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Arsenal.
Man United pia itakuwa na kibarua cha mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya mahasmimu wao wa jiji la Manchester, Man City, mechi itakayopigwa Mei 25 kwenye dimba la Wembley.
Mwaka 2016, Man United ilimtimua aliyekuwa kocha wake, Luis van Gaala licha ya kocha huyo kubeba Kombe la FA lakini Ten Hag amekuwa mwenye kujiamini.
Akizungumzia hali hiyo, Ten Hag alisema kwamba hata wamiliki wa klabu wanajua ni kwa nini kiwango cha timu si kizuri msimu huu.
“Nafikiri wana akili ya kawaida, wanaweza kuona unapokuwa na mambo 32 yanayokurudisha nyuma, unapopoteza wachezaji wanane wa kati, pale wanapoona tunatumia mifumo 13 tofauti katika eneo la kati, wanaona tunapokosa beki wa kushoto, wanaona tulivyo na majeruhi wengi, hayo yote yanaleta matokeo mabaya,” alisema Ten Hag.
Ten Hag alisema kwamba hayafurahii matokeo ya timu yake msimu huu lakini ni lazima awe mkweli kuhusu hali ya wachezaji majeruhi inayomkabili katika kikosi chake.
Hadi sasa tajiri mwenza mpya wa klabu hiyo, bilionea Sir Jim Ratcliffe hajasema lolote kuhusu Ten Hag ingawa kocha huyo alisema hahitaji kura ya wengi kutoka kwenye bodi licha ya kuwapo uvumi mbaya kuhusu majaliwa yake kwenye klabu hiyo.
“Sijali kuhusu uamuzi wowote kama wa kufukuzwa au la, ninafanya kazi ya kuboresha timu na kuipatia maendeleo, hiyo ndiyo kazi yangu hapa,” alisema Ten Hag.
