Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin amezitabiria makubwa timu za Simba na Yanga katika mechi za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na ubora wa vikosi walivyo navyo.
Moallin aliyewahi kuinoa Azam FC msimu uliopita alisema timu hizo mbili zimeimarika mno na kama viongozi pamoja na wachezaji watakuwa makini zinaweza kufika hatua za mwisho ikiwemo kubeba ubingwa wa taji hilo la Afrika.
“Navutiwa sana na ushindani wa Simba na Yanga hasa mtazamo wao wa kutaka kufanya vizuri kwenye mashindano ya Caf, zimeonesha dhamira ya kweli kuanzia kwenye usajili wao na jinsi wanavyocheza, ukweli kama wataendelea hivyo nawaona mbali sana,” alisema Moallin.
Kocha huyo alisema msimu huu tayari amekutana na Yanga kwenye Ligi Kuu NBC na kipigo cha mabao 5-0 alichopewa kilidhihirisha ukubwa na ubora wa timu hiyo na maandalizi yao kuelekea mechi hizo.
Akizungumzia timu yake ya KMC, Moallin alisema wameendelea kuimarika kwa kujenga muunganiko wa wachezaji huku akiamini mapumziko ya wiki mbili waliyoyapata yamemsaidia kukamilisha ambavyo hawakuwa navyo wakati msimu mpya unaanza.
Alisema pamoja na ushindani uliopo kutoka kwa timu za Simba, Yanga na Azam FC lakini anaamini nafasi ya kufanya vizuri na kumaliza ligi kwenye nafasi za juu ni mkubwa kwao kutokana na aina ya wachezaji waliowasajili kwenye kikosi chake.
KMC ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC msimu huu ikiwa na pointi moja katika mechi mbili ilizocheza hadi sasa.