Na mwandishi wetu
Ofisa Habari wa Azam FC, Thabiti Zakaria amesema pamoja na kiwango alichokionesha kipa wao, Zuberi Foba kwenye mechi yao dhidi ya Yanga lakini anapaswa kupewa nafasi ili azidi kuimarika.
Akitolea mifano ya Aishi Manula, Farid Mussa na Bakari Kimwaga miongoni mwa wachezaji wanaowika nchini alifafanua mechi zao za kwanza wakati wapo Azam waliumana na Yanga lakini kila mmoja anafahamu ubora wao kwa sasa.
“Aishi Manula (anayekipiga Simba) ambaye leo ni Tanzania One mechi yake ya kwanza ilikuwa ya Ngao dhidi ya Yanga mwaka 2013 na tulifungwa, Farid Mussa (sasa yupo Yanga), Bakari Kimwaga hawa walianzia mechi zao za kwanza wakicheza na Yanga, ni mechi kubwa kwao lakini leo wanafahamika vizuri.
“Kwa hiyo suala isiwe Foba sana kwa maana wachezaji lazima wacheze ndio wakue na wachezaji wengine wanaanza kwenye mechi kubwa sana, anaweza akaanza hata kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa hivyo isiwe kitu kikubwa sana,” alisema Zakaria.
Alisema hata mashabiki wanaouliza juu ya kiwango cha kipa huyo wanapaswa kufahamu ili chuma kiwe cha pua lazima kipite kwenye moto mkali kwa maana ya mechi nzito zinamjenga mchezaji ndio maana Foba akapewa nafasi.
Kipa huyo aliyeibuka kwenye timu ya vijana ya Azam, amekuwa gumzo kwenye mechi ya jana ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga waliyofungwa mabao 2-0 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga akikosolewa kwa kwa kinachodaiwa kuwa ni kuonesha kiwango hafifu.