Na mwandishi wetu
Simba imeaga kiume michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya robo fainali kwa kulala kwa mikwaju ya penalti 4-3 mbele ya Wydad Casablanca baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika Simba ikifungwa bao 1-0.
Matokeo ya dakika 90 za mechi hiyo iliyopigwa Ijumaa hii kwenye dimba la Mohamed V, Casablanca nchini Morocco, yalizifanya timu kupigiana penalti zikiwa na sare ya jumla ya bao 1-1.
Hiyo ni baada ya Simba nao kupata ushindi kama huo katika dakika 90 za mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba ikineemeka na bao la Jean Baleke.
Katika mikwaju ya penalti, waliofunga penalti tatu za Simba ni Erasto Nyoni, Saido Ntibazonkiza na Moses Phiri wakati Shomari Kapombe na Clatous Chama walikosa.
Matokeo hayo yanafuta rasmi ndoto za Simba kucheza nusu fainali ya michuano hiyo jambo ambalo mashabiki wake walikuwa wakilisubiri kwa hamu baada ya kupata ushindi wa bao pekee katika mechi ya kwanza.
Katika dakika 90 za mchezo huo, mambo yaliwaharibikia Simba katika dakika ya 25 walipolala kwa bao hilo pekee lililofungwa kwa kichwa na mshambuliaji hatari wa Wydad, Junior Sambou ambaye anatokea nchini Senegal.
Bao hilo lilianzia kwenye mpira wa kona iliyookolewa kabla ya kupigwa krosi ambayo Kapombe pia aliokoa kwa kichwa lakini mpira ukiwa juu, Sambou aliruka na kupiga kichwa kwa nguvu akimzidi ujanja beki wa Simba, Joash Onyango na mpira kujaa wavuni ukimshinda kipa wa Simba, Ally Salim.
Kuingia kwa bao hilo hakukuwakatisha tamaa Simba ambao walipambana kiume ambapo katika dakika ya 33, Ntibazonkiza aliinasa pasi ya Chama na kufumua shuti la chinichini ambalo liliwababatiza mabeki wa Wydad na kuwa salama kwa timu hiyo.
Dakika mbili baadaye Kibu Dennis aliambaa na mpira kwa kasi kabla ya kumpasia Chama ambaye naye alimuunganishia Saido naye hapo hapo akafumua shuti la juu na kama si umakini wa kipa wa Wydad, Simba wangeshangilia bao.
Mashambulizi ya Simba kuna wakati yaliwatuliza mashabiki wa Wydad waliofurika uwanjani ambao baadhi yao kamera ziliwaonyesha wakiwa katika hali ya wasiwasi kutokana na jinsi wachezaji wa Simba walivyopambana na kutawala mchezo wakitaka kusawazisha bao hilo.
Hali hiyo ilionekana zaidi Simba walipopata kona hasa mabeki Onyango na Henock Inonga wakiwa kwenye lango la Wydad wakipambana kuvizia mipira ya juu kwa lengo la kufunga mabao ya vichwa.
Kuna wakati kipa wa Wydad alionekana kama akimkoromea mshambuliaji wake Sambou kwa kushindwa kumdhibiti Inonga wakati wa kuwania mpira wa juu.
Kwa ushindi huo Wydad sasa inasubiri kuumana na mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali kati ya Mamelodi na CR Belouizdad.
Kimataifa Simba yafa kiume Morocco
Simba yafa kiume Morocco
Read also