Na mwandishi wetu
Kipa namba mbili wa Azam FC, Ali Ahmada (pichani) amekwenda Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa goti lake la mguu wa kushoto.
Akizungumza na GreenSports, meneja habari na mawasiliano wa Azam, Thabiti Zacharia ‘Zaka Zakazi’ alisema kipa huyo ameondoka nchini usiku wa kuamkia leo Ijumaa.
“Kipa wetu namba moja kwa sasa Ahmada amekwenda Afrika Kusini kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Vincent Pallotti, Cape Town na baada ya vipimo na kujua ukubwa wa tatizo lake ndio tutajua atakuwa nje kwa muda gani,” alisema Zaka Zakazi.
Ahmada aliumia kwenye mchezo wao walioshinda mabao 5-0 dhidi ya KMC ingawa alicheza mchezo uliofuata dhidi ya JKT Tanzania walioshinda kwa mabao 2-1 na kuzidisha maumivu ya jeraha hilo.
Kipa huyo raia wa Comoro, anakuwa kipa wa pili kwenda Cape Town kufanyiwa matibabu baada ya jana Alhamisi kipa namba moja wa timu hiyo, Idrissu Abdulaye naye kwenda nchini humo kwa matibabu ya bega lake la kushoto.
Zakazi alisema kwa kipindi hiki lango lao litakuwa chini ya kipa namba tatu, Zuber Foba ambaye alipandishwa kutoka kwenye Akademi ya klabu hiyo na alicheza vizuri kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan Kusini iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.