Na mwandishi wetu
Weka kando burudani ya muziki kutoka kwa Zuchu na wasanii wengine na matukio mbalimbali ya kisisimua, ushindi wa mabao 2-0 ambao Simba imeupata jioni ya leo dhidi ya St George ya Ethiopia unabaki kuwa tukio pekee kubwa lililowapa raha mashabiki na kunogesha tamasha la Simba Day.
Ni ushindi ambao si tu unatoa ishara ya usajili mzuri lakini pia ni ushindi ambao unaipa ari timu hiyo na mashabiki wake kabla ya kuwavaa mahasimu wao Yanga Agosti 13 mwaka huu katika mechi ya Ngao ya Jamii, mechi ambayo inaashiria kuzinduliwa rasmi kwa msimu mpya wa 2022/23 wa Ligi Kuu ya NBC.
Zaidi ya hayo ni ushindi ambao unatoa picha ya dhamira ya klabu ya Simba kulirudisha katika himaya yake taji la ligi hiyo pamoja na mataji mengine ambayo imeyapoteza katika msimu wa 2021/22 baada ya kuwa tishio kwa misimu minne mfululizo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 18 mfungaji akiwa ni Kibu Dennis kwa shuti kali na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao hilo.
Dakika 11 baada ya kuanza kipindi cha pili, Simba iliandika bao la pili mfungaji akiwa ni mchezaji mwingine mpya wa timu hiyo, Nelson Okwa kutoka Rivers United ya Nigeria ambaye alifumua shuti kali lililogonga mwamba na mpira kumkuta Clatous Chama.
Chama au Mwamba wa Lusaka kwa mara nyingine alitumia nafasi hiyo kudhihirisha uwezo wake hasa jinsi anavyojiamini na asivyo na papara kwani kabla ya kumpasia mfungaji alipiga chenga kama nne hivi akiwa eneo ambalo pengine angetarajiwa afumue shuti kwa haraka lakini hakufanya hivyo.
Baada ya kupiga chenga ndipo akatoa pasi kwa Okwa ambaye alikuwa karibu na lango la St George na hivyo akausukumiza mpira wavuni kiulaini na kuibua shangwe na nderemo kwa mashabiki wa Simba walioujaza uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 kwa wakati mmoja.
Kimataifa Raha ya Simba Day ushindi
Raha ya Simba Day ushindi
Read also
