Barcelona, Hispania
Kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez amesema kwamba atang’atuka kuinoa timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Xavi, kiungo wa zamani wa timu hiyo pamoja na timu ya taifa ya Hispania, alikabidhiwa mikoba ya kuinoa Barca, Novemba 2021 baada ya kuachana na klabu ya Al Sadd ya Qatar.
Katika msimu wake wa kwanza aliouanzia mwanzo wa 2022-23 aliiongoza timu hiyo kubeba taji la Ligi Kuu Hispania au La Liga lakini kipigo cha jana Jumamosi cha mabao 5-3 dhidi ya Villarreal huenda ndicho kilichomfanya achukue uamuzi huo mgumu.
Kipigo hicho cha nyumbani kimeifanya Barca kuwa nyuma ya vinara wa La Liga mahasimu wao, Real Madrid kwa tofauti ya pinti 10.
“Nimekuwa mtu wa klabu hii, nimejitoa kwa ajili ya klabu hii kuliko hata nilivyojitoa kwa ajili yangu mimi binafsi, nimejitoa kwa kila kitu nilichonacho, na nitaendelea kufanya hivyo ili kuwapa raha mashabiki,” alisema Xavi.
Xavi na Laporta pichani.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 na ambaye alipata mafanikio makubwa enzi zake za uchezaji soka ikiwamo kubeba mataji 25, anatarajia kung’atuka rasmi Juni 30 ingawa bado ana mwaka mmoja zaidi katika mkataba wake.
Xavi ambaye mwaka 2010 alishinda Kombe la Dunia akiwa mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania, amefikia uamuzi wa kutangaza kung’atuka Barca baada ya kufanya mazungumzo na rais wa klabu hiyo, Joan Laporta, makamu wa rais, Rafa Yuste na mkurugenzi wa michezo, Deco.
Uamuzi wa Xavi unamfanya kuwa kocha wa pili katika ligi kubwa za Ulaya kutangaza kuachana na timu katika siku za karibuni, mwingine aliyechukua uamuzi huo ni kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp.