Liverpool, England
Kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp ameuelezea uvumi uliopo kwamba anaelekea kuchukua majukumu ya kuinoa klabu ya Real Madrid ya Hispania kuwa ni upuuzi.
Klopp aliyeamua kuachana na Liverpool mwishoni mwa msimu wa 2023-24 baada ya kuinoa kwa miaka takriban tisa amekuwa akifanya kazi na katika taasisi ya Red Bull ambayo inajihusisha na maendeleo ya soka duniani.
Kocha huyo amewahi kukanusha mpango wowote wa kurejea katika soka la ushindani ingawa amewahi kuhusishwa na mipango ya kurudi Liverpool kwa mara nyingine baada ya kocha aliyemkabidhi kiti hicho, Arne Slot kuwa katika wakati mgumu.
Akiwa Liverpool, Klopp aliiwezesha timu hiyo kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu Engoland na kwa sasa habari kubwa zaidi imekuwa ikimhusisha na Real Madrid mwishoni mwa msimu huu ili achukue nafasi ya kocha wa sasa, Alvaro Arbeloa.
Akizungumzia habari hiyo Klopp amenukuliwa akisema kwamba iwapo Real Madrid wangempigia simu kuhusu jambo hilo kila mtu angekuwa amefahamu kwa wakati huu.
“Lakini habari hiyo ni upuuzi, hawajawahi kunipigia hata mara moja, wakala wangu yuko mnaweza kumuuliza, na hata yeye hawajampigia, kwa sasa sifikirii hilo na bahati iliyoje sina sababu ya kufanya hivyo,” alisema Klopp.
Klopp alisema kwa umri wake amepiga hatua kubwa kimaisha lakini katika kazi ya ukocha bado hajamaliza, hajafikia umri wa kustaafu na akamalizia kwa kuhoji nani anayejua mambo ya miaka ijayo ingawa alisisitiza kwamba hakuna alichopanga.
Real Madrid kwa sasa inapambana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa imefuzu hatua ya 16 bora baada ya kuitoa Man City na inajiandaa kuivaa Bayern Munich katika robo fainali lakini imezidiwa pointi nne na Barcelona katika Ligi Kuu Hispania au La Liga.
