Na mwandishi wetu
Azam FC imetangaza rasmi kufunga usajili wa wachezaji baada ya kusajili wachezaji wanne wapya na keshokutwa wanatarajia kuelekea Tunisia kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao kwa siku 21.
Azam FC imeeleza hayo leo Alhamisi ikizungumza na GreenSports na kufafanua kuwa kutokana na timu bora waliyo nayo msimu uliopita na wachezaji wanne waliowaongeza wanatosha kwa mapambano ya msimu wa 2023-24.
Timu hiyo imefanikiwa kuwanasa kiungo Feisal Salum kutoka Yanga, kiungo mshambuliaji Mgambia, Djibril Sillah (Raja Casablanca), na Wasenegali wawili; mshambuliaji, Alassane Diao (US Goree) na beki wa kushoto, Cheikh Sidibe (Teungueth FC).
Ofisa Habari wa Azam, Zakaria Thabiti alisema: “Tumemaliza, msimu huu usajili ni wachezaji wanne tu, hatuhitaji kuwa na wachezaji wengi sana, kama unavyoona tumeongeza na kocha msaidizi (Mfaransa, Bruno Ferry).
Zakaria (pichani) alisema kwamba lengo lao ni kuifanya timu iwe imara maeneo yote kwa ajili ya ushindani na kutoa burudani msimu ujao maana timu waliyokuwa nayo msimu uliopita ilikuwa bora hivyo walihitaji kuongeza sehemu chache.
Alisema pia wastani wa wachezaji wao wengi walionao sasa wana umri mdogo hivyo wanaweza kuwa nao kwa misimu mingi zaidi na timu kuendelea kuimarika.
Pia alibainisha kuwa timu hiyo itaondoka nchini kuelekea mjini Tunis, Julai 9 ambapo itakaa huko kwa siku 21 kabla ya kugeuza Dar es Salaam Julai 30 kumalizia hatua za mwisho za maandalizi hayo.
Azam katika msimu wa 2023-24 mbali na michuano ya ndani lakini pia timu hiyo itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Soka Azam FC yafunga usajili
Azam FC yafunga usajili
Read also