London, England
Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel amesema uzoefu wao mkubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya utakuwa faida kubwa katika mechi na Arsenal leo Jumanne ingawa nyota wa Arsenal, Gabriel Jesus ameionya timu hiyo akisema kwamba wao si watoto tena.
Timu hizo zinaumana katika mechi ya robo fainali ya ligi hiyo huku Tuchel akisema wanajua namna ya kuiumiza Arsenal ambayo mafanikio yao makubwa katika ligi hiyo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2006 walipofikia hatua ya fainali.
“Tuna uzoefu zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa, ligi hii ni tofauti na Ligi Kuu England (EPL), tunataka kuitumia faida hiyo,” alisema Tuchel.
Tuchel (pichani chini) ambaye ataachana na timu hiyo baada ya msimu huu hata hivyo alisema ni sahihi kwa timu yake kukoselewa kwa kuwa imekosa matokeo bora ikiwamo kwenye Ligi Kuu Ujerumani yaani Bundesliga.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Bayern, Arsenal imekuwa na mwenendo mzuri na ni kati ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kulibeba taji la EPL msimu huu.
Kwa upande wake Jesus amewaonya Bayern akisema Arsenal si watoto tena na sasa wanawania kufikia hatua ya nusu fainali ambayo mara ya mwisho waliifikia mwaka 2006.
“Kama nitaona jambo naweza kuwaambia na kuwasaidia (wachezaji wenzangu) nitafanya hivyo lakini sidhani kama hapa bado kuna watoto kila mmoja ameshacheza hatua kubwa kwenye soka, Kombe la Dunia, ligi kuu na sasa ligi ya mabingwa, kwa hiyo nafikiri kila mmoja wetu yuko tayari kuisaidia Arsenal,” alisema Jesus.
Jesus alisema msimu uliopita walicheza soka la uhakika katika sehemu kubwa ya mwanzo ya msimu hadi Januari na baada ya hapo hali ikawa kidogo si nzuri, msimu huu imekuwa kinyume chake.
Bayern katika mechi ya leo itamtegemea Harry Kane kuongoza mashambulizi, mshambuliaji ambaye tayari ameonesha ubora wa kuzifumania nyavu katika msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Tottenham.
Hadi sasa Kane ana mabao 38 katika mechi 37 na hivyo usajili wake ulioigharimu Bayern Dola 130 milioni umeonekana kulipa licha ya kiujumla timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri.
“Kila mtu anajua ubora wa Harry Kane, kwangu mimi huyu ni mfungaji bora duniani, kwa hiyo ni jambo kubwa kucheza na timu yenye wachezaji wa aina hii lakini tunataka kumnyamazisha, na baada ya hapo tujaribu kushinda mechi,” alisema Jesus.
“Pia si Harry Kane pekee, lakini kuna wachezaji wengi kama Sane (Leroy) rafiki yangu wa zamani, Musiala (Jamal) Coman, Muller (Thomas) Gnabry, ni wengi, wana wachezaji wa hadhi ya juu,” alisema Jesus.
Mechi za leo Jumanne Ligi ya Mabingwa Ulaya
Arsenal v Bayern Munich
Real Madrid v Man City