New York, Marekani
Wayne Rooney ameamua kuachia ngazi katika nafasi yake ya kocha mkuu wa timu ya D.C United ya Marekani baada ya timu hiyo kushuka daraja.
Wikiendi hii imekuwa si nzuri kwa D.C United baada ya kufungwa mabao 2-0 na timu ya New York City FC katika mechi yake ya mwisho ya msimu lakini matokeo ya mechi nyingine yanamaanisha kwamba timu hiyo haina nafasi tena ya kufuzu na kuendelea na ligi kubwa.
Mara tu baada ya mechi hiyo, taarifa ya klabu hiyo ilieleza kwamba imeamua kuachana na Rooney baada ya pande mbili kuafikiana katika hilo.
“Tumezungumza na Wayne na kukubaliana kwamba ni jambo zuri kwetu sote kuachana kwa wakati huu,” alisema ofisa mtendaji mkuu wa D.C United, Jason Levien.
“Tunamshukuru Wayne Rooney kwa yote aliyoyafanya katika klabu yetu na kwa mchezo wa soka katika taifa letu, kwanza akiwa mchezaji na nahodha na hivi karibuni akiwa kocha, anabaki kuwa mtu muhimu katika familia ya D.C. United,” alisema Jason Levien.
“Nafikiri huu ni wakati sahihi kwangu kurudi England, kinachofuata baadaye sikijui,” alisema Rooney mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya England na klabu za Man United na Everton.
