Na mwandishi wetu
Yanga imewashusha mahasimu wake, Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa KMC mabao 4-1 katika mechi iliyochezwa Jumapili hii Novemba 9, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi nne, ikishinda tatu na sare mechi moja wakati Simba waliokuwa kileleni na sasa wanashuka hadi nafasi ya pili wana pointi tisa katika mechi tatu.
KMC ambao msimu huu wameuanza vibaya, walionekana kuwa tofauti mwanzoni kiasi cha kuzifanya timu kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1 huku Yanga wakiwa wa kwanza kupata bao kabla ya KMC kusawazisha.
Yanga walianza kuzichana nyavu za KMC katika dakika ya 36 kwa bao la Maxi Nzengeli ambaye alifunga bao hilo baada ya kushirikiana vyema na Pacome Zouzoua.
Zikiwa zimebaki dakika nne timu kwenda mapumziko, KMC walizawazisha kupitia kwa Daruwesh Saliboko ambaye aliuwahi na kuujaza wavuni mpira uliopigwa na Rashid Chambo kabla ya kuokolewa na kipa wa Yanga, Djigui Diara.
Yanga waliongeza bao la pili dakika ya 73 mfungaji akiwa ni Pacome baada ya kuinasa krosi ya Israel Mwenda na wakati KMC wakiwa katika mapambano ya kutaka kusawazisha walifungwa mabao mawili na Andiy Boyeli dakika za 81 na 90.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo mambo hayaonekani kuwa mazuri kwa matajiri, Azam FC ambao wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC.
Soka Yanga yaacha maumivu KMC
Yanga yaacha maumivu KMC
Read also
