
NEW YORK, MAREKANI
Mwaka 2002 staa wa filamu Ben Affleck na mwanamuziki Jeniffer Lopez au J.Lo walikuwa gumzo duniani hadi kubatizwa jina la Super Couple na baadaye Bennifer ikiwa ni ufupisho wa majina yao .
Kila walipokwenda, kila walichofanya kilikuwa habari na haikushangaza kuwakuta kila mara wakiwa kwenye vyombo vya habari na kuwa gumzo duniani kote. Ukweli ni kwamba wawili hawa walikuwa kivutio na waliteka hisia za wapenzi wa filamu, muziki na wengineo waliopenda kusikia habari zao.
Hata hivyo kumulikwa kwa mambo yao na vyombo vya habari kukageuka kero na ikatosha kuwa sababu ya kuachana kwao na kuwaacha vinywa wazi mashabiki wao waliokuwa wakiisubiri kwa hamu ndoa ya ma-Super Couple hawa ambayo tayari ilianza kunukia.
Ndoa hiyo iliyopangwa kufungwa Septemba 14, 2003 iliota mbawa kwa taarifa iliyotolewa siku nne kabla ya tukio hilo sababu ikielezwa kuwa ni kukerwa na namna ambavyo vyombo vya habari vilikuwa vikiwanyima utulivu kwa kuyashupalia mambo yao na kila sehemu waliyokwenda.

J.Lo ambaye pia ameigiza filamu kadhaa, alikiri kwamba kuachana na Ben Affleck ni tukio la kwanza kubwa lililomuumiza mno moyo.
Baada ya kuachana, Affleck alianza kutoka na rafiki yake wa zamani, Jennifer Garner na kufunga naye ndoa mwaka 2005, ndoa iliyobarikiwa watoto watatu lakini wawili hao waliachana mwaka 2018.
J.Lo naye alirudiana na mpenzi wake wa zamani, Marc Anthony na kufunga naye ndoa Juni 2004 na mwaka 2008, J.Lo alijifungua watoto wawili mapacha, Maximilian David na Emme Maribel lakini ndoa yake na Marc nayo ilivunjika mwaka 2011.
Julai mwaka huu, J.Lo alithibitisha kile alichokisema mwaka 2004 kwamba kuachana na Affleck kulimuumiza mno moyo na hatimaye sasa amekiri kurudiana naye baada ya uvumi kuenea mapema mwaka huu kwamba Super Couple iliyotingisha 2002 hadi 2004 inatudi tena.
Wakati wanaachama mwaka 2004, Affleck ndio kwanza alikuwa mkaka wa miaka 32 wakati J.Lo alikuwa mdada wa miaka, 35 leo hii wanarudiana Affleck ni mtu mzima mwenye miaka 49 wakati J.Lo ni mama wa miaka 52.
