Barcelona, Hispania
Klabu ya Barcelona ‘Barca’ ya Hispania imekamilisha usajili wa mshambualiaji wa kimataifa wa Misri, Hamza Abdelkarim (pichani) kutoka klabu ya Al Ahly kwa ada ya Euro milioni 1.5.
Abdelkarim, 18, awali alijiunga na Barca mwezi Januari kwa mkopo lakini klabu hiyo imeamua kufanya usajili wa kudumu baada ya kuridhishwa na kiwango chake kwenye timu mbili za vijana za klabu hiyo.
Mafanikio ya Abdelkarim kwenye timu za Barca yamemfanya aitwe kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Misri inayoshiriki fainali za Kombe la Dunia na atavaa jezi namba 9 akishirikiana na Omar Marmoush na Mohamed Salah kwenye safu ya ushambuliaji.
Abdelkarim alicheza kwa mara ya kwanza kwenye timu ya taifa ya Misri dhidi ya Russia, mechi iliyopigwa Mei 28, 2026 na Misri kushinda kwa bao 1-0 na hivi karibuni alicheza mechi nyingine dhidi ya Brazil akitokea benchi, mechi ambayo Misri ililala kwa mabao 2-1.
Katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendela katika nchi za Canada, Mexico na Marekani, Misri au Pharaohs wapo Kundi G na timu za New Zealand, Iran na Ubelgiji ambao wanacheza nao mechi ya kwanza Jumatatu Juni 15, 2026.
Abdelkarim alijiunga na miamba ya Misri, Al Ahly mwaka 2020 kabla ya kupanda daraja hadi kikosi cha kwanza ambapo alionekana mara ya kwanza Februari 2025 akitokea benchi katika mechi dhidi ya Petrojet.
Aliichezea Ahly jumla ya mechi tisa katika mashindano yote kabla ya kujiunga na Barca mapema mwaka huu.
Kimataifa Barca yamsajili straika dogo wa Misri
Barca yamsajili straika dogo wa Misri
Read also
