Na mwandishi wetu
Bao pekee la Aziz Ki limeiwezesha Yanga kunyakua pointi tatu muhimu za ugenini katika mechi ya Ligi Kuu NBC dhidi ya Mtibwa Sugar na kuifanya timu hiyo iendelee kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa imefikisha pointi 50.
Kwa ushindi huo uliopatikana leo, maana yake ni kwamba Yanga sasa inakuwa imeipiku Simba iliyo nafasi ya pili kwa jumla ya pointi sita, timu zote hizo zimecheza mechi 19 ingawa Simba inajivunia mabao mengi ya kufunga, ina mabao 47 dhidi ya 37 ya Yanga.
Aziz Ki alifunga bao hilo katika dakika ya 26 baada ya kuupiga mpira wa adhabu kwa guu lake la kushoto na mpira huo kumgonga kipa wa Mtibwa kabla ya kujaa wavuni upande wa kushoto akimuacha kipa huyo akiwa ameduwaa.
Yanga hata hivyo itabidi ijilaumu kwa kufanya mashambulizi mara kadhaa ya mfululizo ambayo hata hivyo hayakuweza kuzaa mabao, mfano dakika ya 71 Aziz Ki aliambaa na mpira na kumpasia Fiston Mayele ambaye shuti lake la chinichini halikuzaa bao.
Dakika mbili baadaye Tuisila Kisinda alipiga krosi ambayo Mayele aliunganisha kwa kichwa lakini mpira aliopiga ‘haukuwa na macho’ na dakika moja baadaye tena, Aziz Ki alifanya juhudi binafsi kwa kuambaa na mpira kabla ya kufumua shuti la juu ambalo kipa wa Mtibwa aliliona na kuokoa mpira ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kwa mara nyingine Yanga imecheza mechi ya pili ya ligi bila ya kuwa na kiungo wake mahiri, Feisal Salum au Fei Toto ambaye habari zisizo rasmi zinada kwamba ameweka shinikizo akitaka apate baraka za klabu hiyo ili ajiunge na Azam.
Azam, v Mbeya City
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Azam imeipa kipigo kikali Mbeya City kwa kuichapa mabao 6-1 ikineemeka na mabao ya Abdul Sopu aliyefunga mawili, Prince Dube, Keneth Mugune, Idd Nado na Cleophance Mukandala wakati bao pekee la Mbeya City lilifungwa na Richardson Ngodya.
Ushindi huo unaifanya Azam kujiimarisha katika nafasi ya tatu ikiwa imefikisha pointi 40 katika mechi 19 na mabao 33 ya kufunga.
Soka Aziz Ki aipa pointi 3 Yanga, Azam yaua
Aziz Ki aipa pointi 3 Yanga, Azam yaua
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
