London, England
Hatimaye Chelsea imefanikiwa kumsajili beki wa kati, Wesley Fofana kutoka Leicester City kwa ada ya Pauni 70 milioni na mkataba wa miaka saba.
Fofana mwenye umri wa miaka 21 na ambaye usajili wake umekuwa gumzo hivi karibuni, pia ni mchezaji wa timu ya vijana chini ya miaka 21 ya Ufaransa, alitua England mwaka 2020 na kujiunga na Leicester akitokea Saint-Etienne ya Ufaransa na hadi sasa amecheza mechi 37 za Ligi Kuu England.
Msimu wa 2021/22 kidogo ulikuwa mgumu kwa Fofana baada ya kuumia mguu wakati akiiwakilisha Leicester katika mechi ya kirafiki dhidi ya Villarreal ya Hispania na hivyo kujikuta akikosa mechi saba za Ligi Kuu England.
‘Siku mbili hizi zimekuwa kubwa mno kwangu na nina furaha kwa jambo hilo, nimefanya mazoezi asubuhi hii na timu hii, ni timu ya ndoto yangu, nina shauku kubwa ya kuanza kucheza mechi kwa ajili ya klabu hii na mashabiki,” alisema Fofana.
“Niko hapa kwa ajili ya kushinda mataji, taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu England, FA, Carabao na kila kitu, nimekuja hapa kwa ajili ya ushindi pamoja na kuijenga klabu hii ishinde mataji, kwa hiyo niko hapa ili kuendeleza hayo.” alisema.
Katika usajili huo, kuna nyongeza ya fedha ambazo Chelsea watatakiwa kutoa lakini fedha hizo zote kwa pamoja haziwezi kuzidi Pauni 80 milioni ambazo Manchester United ililipa mwaka 2019 kwa ajili ya kumsajili aliyekuwa beki wa Leicester, Harry Maguire ambaye aliweka rekodi ya dunia ya ada kubwa ya uhamisho kwa mabeki.
Fofana hata hivyo naye anabaki kuwa mmoja wa mabeki waliosajiliwa kwa bei mbaya katika Ligi Kuu England akiwa amezidiwa na Maguire na Virgil van Dijk ambaye mwaka 2017 alijiunga na Liverpool kwa ada ya Pauni 75 milioni.
Kwa rekodi za ujumla za mabeki waliosajiliwa kwa bei mbaya katika Ligi Kuu England, Fofana anashika nafasi ya 12 lakini huenda akajikuta akiangukia katika nafasi ya 13 baada ya Manchester United kukamilisha usajili wa Mbrazil, Antony ambaye usajili wake kwa ujumla unatajwa kufikia ada ya Pauni 81.3 milioni.
Kimataifa Hatimaye Fofana asaini Chelsea
Hatimaye Fofana asaini Chelsea
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
