Na Hassan Kingu
Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo. Je nini kinafuata baada ya uamuzi huo?
Katika taarifa iliyopatikana leo, Barbara ametaja sababu mbili za kujiuzulu, moja ni kuipa nafasi bodi mpya itakayochaguliwa katika uchaguzi ujao kuchagua mtendaji mpya na sababu ya pili ni kujipa nafasi ya kutimiza ndoto na fursa nyingine nje ya Simba
Sababu ya kwanza inamfanya mtu kuamini kwamba Barbara amechukua uamuzi huo huenda amebaini kwamba hatokuwamo kwenye bodi ijayo au bodi ijayo haitompa nafasi ya kuendelea na uongozi na ndio maana ameamua kukaa pembeni.
Sababu ya pili ni ya msingi na yenye mantiki lakini pia inaweza kumfanya mtu kujiuliza Barbara kwa muda ambao amekuwa ndani ya Simba amefanikisha nini kiasi kwamba ametosheka na sasa anafikiria kukimbizana na ndoto nyingine? Au yeye amefaidika na nini ndani ya Simba na sasa anaona inatosha ni vyema aende kwenye changamoto nyingine
Kwa muda mrefu moja ya sifa ambayo Barbara amekuwa akihusishwa nayo ni uwezo wa kusimamia na kuratibu mambo, hili linaweza kuwa mafanikio kwa Simba si Barbara kwani inaonekana ni sifa yake, ni uwezo ambao anao na ameudhihirisha akiwa Simba, hajajifunzia Simba.
Kwa maana nyingine ni Simba ndiyo iliyonufaika na sifa hii ya Barbara, kesho na keshokutwa akija CEO mwingine anatakiwa pamoja na sifa nyingine anazoweza kuwa nazo sifa ya kuratibu na kusimamia mambo kwa kasi ya Barbara ni kitu kingine muhimu atakachoangaliwa, mambo yakidorora atakumbukwa Barbara.
Barbara pia anatajwa kufanya kazi nzuri ya kui-brand Simba ndani na nje ya nchi, hadhi ambayo Simba inayo ya kuwa moja ya klabu kongwe na yenye wanachama wengi kati ya klabu kongwe za Afrika, imetumiwa vyema na Barbara katika kuikuza zaidi hadhi hiyo.
Sambamba na yote hayo, Barbara pia amejipatia uzoefu, kwa muda aliokaa Simba bila shaka amejifunza mengi, amepata uzoefu ambao utamfaa kwingine si ndani tu hata nje ya nchi, naamini Barbara anaweza kwa sasa kwenda kuwa CEO wa klabu nyingine yoyote kubwa Afrika au hata nje ya Afrika. Tusishangae kukisikia yuko Afrika Kusini, Ghana na kwingineko, Simba ikiwa daraja la kumfikisha huko.
Je Barbara kafanikiwa akiwa Simba? Upande mmoja kafanikiwa katika hayo niliyoyataja lakini katika mpira bado hakuna jipya lililopatikana katika uongozi wake, nilidhani angeondoka baada ya Simba kubeba taji la Afrika au kufikia fainali ya michuano ya Afrika hapo tungesema amefanikiwa.
Nasema hivyo kwa sababu ndoto hii imewahi kuzungumzwa na watu mbalimbali akiwamo mtu mmoja mzito ndani ya Simba na uwapo wa Barbara baadhi yetu tulidhani ungechangia kuitimiza ndoto hiyo kumbe sivyo na Barbara hatimaye anaondoka.
Na je nini kinafuata baada ya kuondoka kwake au nani mwingine anafuata? vipi kuhusu udhamini? na vipi kuhusu habari zinazosikika zisizo rasmi kwamba hata masuala ya kiuchumi ndani ya Simba ni kama vile kumekuwa dalili za kuyumba? Muda utaeleza yote.
Soka Kujiuzulu kwa Barbara Simba, nini kinafuata?
Kujiuzulu kwa Barbara Simba, nini kinafuata?
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
