Na mwandishi wetu
Wawakilishi wa Taanzania, Simba wameanza vibaya mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulala kwa bao 1-0 mbele ya Horoya FC ugenini mjini Conakry, Guinea.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa General Lasana Conte, wenyeji walipata bao hilo dakika ya 18 likifungwa kwa kichwa na Pape Ndiaye aliyeunganisha mpira wa kona akimzidi ujanja beki Henock Inonga.
Simba pamoja na kuonyesha uhai lakini dakika ya 72 bado kidogo waadhirike baada ya Horoya kupata penalti lakini mpigaji Ndiaye alishindwa kumchambua kipa Aishi Manula ambaye aliutoa mpira huo na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Manula mbali na kuokoa penalti hiyo iliyotolewa baada ya Joash Onyango kuunawa mpira, pia ndiye aliyekuwa mwiba kwa Horoya kwa kuokoa michomo kadhaa ambayo ingeweza kuwapa Horoya mabao mengine.
Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ katika eneo la kati aliwapanga viungo wakabaji Ismail Sawadogo, Muzamiru Yassin na Kanoute na timu hiyo kujikuta ikiwashambulia wapinzani wao mara chache.
Katika kuimarisha safu ya ushambuliaji, Robertinho aliwatoa, Pape Sakho na Jean Baleke na nafasi zao kuchukuliwa na Kibu Dennis na nahodha John Boco, mabadiliko yaliyoonekena kuipa uhai safu ya ushambuliaji.
Simba ilifanya mashambulizi kadhaa lakini nahodha Bocco na Kibu walishindwa kuzitumia vizuri nafasi walizopata ambazo zingeweza kubadili matokeo ya mchezo huo.
Nafasi mojawapo ni ile ya Bocco baada ya kuunganishiwa pasi murua na Clatous Chama hadi kuwainua mashabiki walioamini tayari timu yao imepata bao lakini mshambuliaji huyo alishindwa kufunga na mpira kuokolewa na beki wa Horoya, Samasekou.
Kwa matokeo hayo ya Kundi C, Simba sasa inashika nafasi ya tatu katika kundi hilo linaloongozwa na Raja Casablanca yenye pointi tatu na mabao matano ikifuatiwa na Horoya yenye ponti tatu na bao moja na iliyo mkiani ni Vipers ya Uganda.
Simba baada ya matokeo hayo sasa inasubiri kuumana na Raja Casablanca mechi itakayopigwa Februari 18 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kimataifa Simba yaanza vibaya Afrika
Simba yaanza vibaya Afrika
Read also